Yanga uso kwa uso na Nabi Sauzi

YANGA SC itacheza dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini inayonolewa na kocha Nasreddine Nabi Julai 28 mwaka huu.

Mchezo huo umepangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Toyota uliopo Bloemfontein nchini Afrika Kusini ukiwa ni wa michuano ya kirafiki ya Kombe la Toyota.

Taarifa ya Kaizer imethibitisha uwapo wa mechi hiyo ikieleza: “Kaizer Chiefs watakuwa wenyeji wa Yanga katika mchuano wa kwanza wa Kombe la Toyota utakaochezwa kwenye Uwanja wa Toyota mjini Bloemfontein Julai 28, 2024.”

Rais wa Yanga, Eng. Hersi Said, amezungumzia mwaliko huo kwa kusema: “Sisi kama Yanga tunafurahishwa sana na mwaliko huu wa kushiriki katika Kombe la Toyota 2024.

“Mchezo huu unaendeleza uhusiano kati ya timu zetu kubwa mbili barani Afrika ambao ulianza mwaka jana tulipowaalika Kaizer Chiefs kushiriki katika Tamasha la Wiki ya Mwananchi. Tunafurahia mwaliko huu na tunaahidi kutoa mchezo wa ushindani utakaotusaidia kujiandaa kwa msimu mpya wa 2024/25.”

Kikosi cha Yanga leo kimeingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na pre-season kikiwa na mastaa wote wapya waliosajiliwa kipindi hiki.

Hadi kufikia leo mchana, Yanga ilikuwa imewatambulisha wachezaji wapya wanne, Clatous Chama aliyetokea Simba, Prince Dube (Azam), Chadrack Boka (FC Lupopo) na Khomeiny Aboubakar (Ihefu).

Related Posts