Dar es Salaam. Raia wa Burundi, Gervas Ndayitwayeko (26), amehukumiwa kulipa faini ya Sh500,000 au katumikia kifungo cha mwaka mmoja jela, baada ya kupatikana na hatia ya kuishi nchini Tanzania bila kuwa na kibali.
Ndayitwayeko, amehukumiwa adhabu hiyo leo Jumatatu Julai 8, 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kukiri shtaka lake na mahakama kumtia hatiani.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo ameshindwa kulipa faini hiyo. Amepelekwa gerezani.
Kabla ya kupewa adhabu hiyo, mshtakiwa huyo, alijitetea kuwa anaomba apunguziwe adhabu kwa sababu alikuja kutafuta maisha.
“Naomba nipunguziwe adhabu, nilikuja kutafuta kazi na vilevile ni mkosaji wa mara ya kwanza, hivyo Mahakama inipunguzie adhabu” amedai mshtakiwa.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya amesema mshtakiwa ametiwa hatiani kama alivyoshtakiwa.
“Kutokana na mshtakiwa kukiri shtaka lake mwenyewe bila kulazimishwa, Mahakama inaona ni mkosaji kwa mara ya kwanza, lakini pia imezingatia kuwa upande wa mashtaka hawana kumbukumbu za makosa ya nyuma, Mahakama ina kuhukumu kulipa faini ya Sh500,000 na ukishindwa utatumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani,” amesema Hakimu Lyamuya.
Awali, Wakili kutoka Idara ya Uhamiaji, Mohamed Mlumba ameiomba Mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa.
Akimsomea hati ya mashtaka, Wakili Mlumba alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Juni 20, 2024 eneo la Temeke katika Ofisi ya Uhamiaji.
Amedai siku hiyo, mshtakiwa akiwa raia wa Burundi alikutwa akiishi nchini bila kuwa na nyaraka yoyote ya inayoonyesha kuwa ni raia wa Burundi, huku akijua kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.