Geita. Mkazi wa Nyankumbu, Wilaya na Mkoa wa Geita, Elizabeth Vicent (30) amejifungua watoto wanne ikiwa kama majibu ya maombi yake kupata watoto zaidi na matamanio ya mumewe ya kupata watoto pacha.
Mwanamke huyo ambaye alikuwa watoto wengine watatu, alijifungua pacha hao Julai 3, 2024 katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Geita na watoto hao bado wako chini ya uangalizi wa madakatari katika hospitali hiyo kwa kuwa walizaliwa kabla ya wakati (njiti).
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo, Elizabeth amesema baada ya kujifungua watoto watatu, hakupata ujauzito kwa miaka mitano, jambo lililomfanya afanye maombi ya kuomba Mungu amsaidie kupata tena ujauzito.
“Nilikaa miaka mitano bila kupata ujauzito, nikawa natamani kupata ujauzito. Mume wangu alikuwa anatamani mapacha, nikawa namwambia tumuombe Mungu. Kuna siku kanisani Mchungaji alikuwa akisali, akasema anayetaka mapacha apokee na akasema anayetaka mapacha akanunue nguo za mapacha. Nilienda sokoni kununua nguo za pacha wawili, nikazitunza kwa miaka miwili ndani bila kuwa mjamzito.
“Sisi tuliomba mapacha tukijua ni watoto wawili, lakini Mungu katubariki watoto wanne. Nilianza kliniki mimba ikiwa na miezi miwili, ilipofika miezi minne, tumbo lilikuwa kubwa. Daktari akashauri nifanye ultrasound ili niangaliwe na nilipofanya wakagundua nina watoto watatu,” amesema.
Mwezi uliofuata, mama huyo aliyefanyiwa upasuaji baada ya ujauzito kufikia umri wa wiki 31, amesema akiwa mjamzito alianza kulemewa mimba ikiwa na miezi miwili na kutokana na tumbo kuwa kubwa kupita kiasi.
Amesema ilipofika miezi minne alifanyiwa ultrasound tena na uchunguzi ukabaini ana watoto wanne tumboni.
Kutokana na tumbo kuwa kubwa, amesema alipewa rufaa ya kwenda hospitali ya mkoa ambapo baada ya kuchunguzwa, daktari alimweleza kutokana na uzito, hataweza kuendelea na ujauzito huo hadi miezi tisa na akashauri afanyiwe upasuaji kuwatoa watoto hao wakiwa na wiki 31 badala ya wiki kati ya 37-42.
Hata hivyo, mwanamke huyo amesema pamoja na baraka hiyo ya watoto, sasa wanawaza namna ya kuwalea kutokana na kutokuwa na uwezo wa kununua maziwa ya kuwatosha pamoja na changamoto ya nguo na ‘pampasi’.
Akizungumzia tukio hilo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Geita, Thomas Maphuru amesema afya ya mama na watoto inaendelea vizuri na kwamba watoto hao kwa sasa wana kilo 0.9 (gramu 900) huku mdogo akiwa na kilo 0.8 (gramu 800).
Amesema watoto hao wataendelea kukaa hospitali hadi pale watakapofikisha kilo mbili au zaidi na kuweza kunyonya vizuri.
Hilo sio tukio la kwanza kwa mwanamke kujifungua watoto zaidi ya wawili mkoani Geita, baada ya Desemba 7, 2022, Happines Yohana (30) kujifungua mapacha wanne katika Kituo cha Afya Katoro na Machi 4, 2024 Rebeka John (27), mkazi wa Ikurwa kujifungua watoto watatu katika Kituo cha Afya Nyankumbu.