Aziz Ki, Yanga bado pazito, Hersi afunguka

Rais wa Yanga, Hersi Said amesema kuwa kiungo nyota wa timu hiyo, Stephane Aziz Ki bado hajasaini mkataba mpya wa kuitumikia timu hiyo ingawa wapo katika nafasi nzuri ya kumbakisha.

Akizungumza nchini Afrika Kusini leo Julai 8, 2024, Hersi amesema kuwa klabu inapambana kwa juhudi kubwa kumshawishi mchezaji huyo abakie na yeye mwenyewe anaonyesha dalili za kutamani kubaki ingawa nguvu ya fedha inaweza kumuondoa.

“Ni mkakati wa klabu kuhakikisha mchezaji anabaki na majadiliano yanaendelea vizuri na hapana shaka tutarudi kufanya utambulisho ingawa kuna klabu nyingi zinamhitaji mchezaji.

“Hivyo majadiliano yanaendelea na ninaweza kusema kuna nafasi kubwa kwa mchezaji kubakia lakini hatujakamilisha.

“Aliweka wazi kuwa anataka kubaki unajua nilimsaini miaka miwili iliyopita na nilimsajili kutoka Asec Mimosas na nikamueleza kuhusu ‘project’ yangu na nani nataka waipeleke klabu katika ngazi za juu na akawa sehemu muhimu ya program na mpango ambao upo hi vyo majadiliano yakawa yaleyale na alisema wazi kuwa nahitaji kubaki hapa na kuipeleka Yanga katika ngazi ambazo unataka ifike.

“Lakini mpira ni biashara sasa unaweza kusema unataka kubaki lakini hali ya kifedha ikabadilisha mawazo kwa hiyo naweza kusema ni 60/40 (uwezekano wa kubaki),” alisema Hersi.

Ki alitoa mchango mkubwa kwa Yanga msimu uliopita ilipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ambapo aliibuka kinara wa kufumania nyavu akipachika mabao 21.

Idadi hiyo ya mabao ilimuwezesha nyota huyo kutoka Burkina Faso kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu.

Msimu wake wa kwanza kuichezea Yanga ambao ni 2022/2023, Aziz Ki alitoa mchango mkubwa katika kuiwezesha timu hiyo kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Related Posts