Tabora. Katika hali isiyo ya kawaida, Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata) katika Kata ya Mtendeni, Manispaa ya Tabora, limeazimia kumuondoa katika nafasi yake, sheikh wa kata hiyo, Bakari Sikonge kwa madai ya kufungisha ndoa mara mbili pamoja, kufuja fedha za msikiti na kutumia madaraka yake vibaya.
Hatua hiyo imefuata baada ya kuwepo kwa malalamiko ya baadhi ya wananchi kuhusu sheikh huyo anayedaiwa kufungisha ndoa kiholela na kutotoa nafasi kwa wanandoa kusuluhisha migogoro yao kabla ya kuwafungisha ndoa nyingine.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 9, 2024, Imamu wa Msikiti wa Muuminuna Tabora, Habib Juma Farhan amesema wamefikia uamuzi wa kutangaza kuacha kufanya kazi na sheikh huyo kutokana na matendo yake kuwa kinyume na maadili ya dini hiyo ikiwemo ubadhilifu wa fedha.
“Mkutano huu wa leo umeazimia kumsimamisha sheikh huyo wa Kata ya Mtendei kuanzia leo hadi pale ofisi ya sheikh wa mkoa itakapoteua jina lingine la sheikh wa kata kwa kuwa amefanya vitendo ambavyo ni kinyume na maadili ya dini yetu,” amesema.
Sheikh Sikonge anadaiwa kutumia madaraka yake vibaya ikiwemo kuozesha ndoa mara mbili, kutumia madaraka yake vibaya kwa kuwafuta kazi walioko chini yake pamoja na kuuza nyama za ng’ombe za swadaka zilizotolewa na waturuki kwa waislamu kugawiwa bure, badala yake akaziuza, kilo moja Sh1,000.
Mjumbe wa Bakwata, Kata ya Mtendeni, Abdulahman Mussa amesema lengo lao si kuona damu ikimwagika bali ni kutengeneza na wanachotaka ni mamlaka zinazohusika kuhakikisha amewekwa pembeni.
“Sheikh wa kata yetu, Bakari Sikonge, kwa aliyoyafanya itoshe tu viongozi wetu wafanye uwajibikaji tujitambue, tubadilike tuache mazoea, lengo ni kutengeneza na siyo kubomoa. Tunachoomba viongozi wetu wa juu watuwekee huyu mtu pembeni, hatutaki kuleta ugomvi baina ya nafsi yake na nafsi zetu sisi,” amesema.
Alipotafutwa kuzungumzia jambo hilo, Katibu wa Bakwata Mkoa wa Tabora, Mohamed Abeid amesema uamuzi uliotolewa baada ya kikao cha baraza la masheikh mkoa ni halali na sheikh huyo ameondolewa.
“Changamoto hizo tulizipata kupitia kwa waumini wetu kuwa kuna changamoto ya sheikh wa kata hiyo, Bakari Sikonge kwamba anatumia madalaka vibaya, pia amekuwa akifuja fedha za waamini na mkoa umeelekeza kiitishwe kikao cha mashekhe kujadili suala hilo ili lipatiwe ufumbuzi,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi kuhus tuhuma zinazomkabili, Sheikh Sikonge amesema hawezi kuzungumza lolote kwa kuwa suala hilo tayari lipo kwa viongozi wa ngazi ya mkoa.
“Siwezi kuzungumza lolote, wao kama wameleta tuhuma kwako ni wao kwa kuwa Bakwata ina taratibu zake, jambo hili liko kwa viongozi wa juu na nikisema lolote nitakuwa nimekiuka taratibu za viongozi wangu, lakini naendelea na majukumu yangu hadi sasa,” amesema.