EWURA YAPONGEZWA KATIKA JITIHADA ZA KUDHIBITI HUDUMA ZA NISHATI NCHINI

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba amesema ubora wa umeme kwa siku za hivi karibuni zimeimarika hivyo changamoto ya kukatikakatika kwa sasa hakuna, wanaendelea kuboresha na niwajibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kusimamia.

Ameyasema hayo leo Julai 9, 2024 wakati alipotembelea banda EWURA kwenye Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.

Amesema bei ya umeme kwasasa ipo chini ukilinganisha na mataifa mengine ya Afrika Mashariki na pia ameipongeza EWURA kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma inayostahili kwenye upande wa nishati.

Katika upande wa gesi asilia, EWURA wamekuwa wakifuatilia, wamekuwa wakitoa leseni kwa wale ambao wanajenga vituo vya CNG pamoja na vituo vya mafuta pamoja na kusimamia kuhakikisha huduma zinazotolewa na vituo hivyo zinakidhi mahitaji ya jamii.

“Wizara tupo kwaajili ya kuhakikisha EWURA anafanya kazi yake kulingana na sheria na sera zilizpo na kumuwezesha kuweza kutekeleza majukumu yake katika mazingira yanayokubalika ndani ya sekta”. Amesema

Amesema kwa upande wa Gesi asilia, EWURA inasaidia kutoa Leseni hasa kwa wale wanaojenga vituo vya (CNG) kwenye maeneo mbalimbali nchini, lakini pia EWURA inahakikisha ile huduma inayotolewa inakidhi mahitaji ya Jamii.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ewura James Andilile amesema wameingia mkataba na TANESCO kwalengo la kusimamia utendaji kazi wao ili kuboresha upatikanaji wa Umeme na hivyo Serikali inafanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya Nishati ili kuhakikisha sekta hiyo inaimarika.

Pamoja na hayo amewakaribisha wawekezaji kutoka katika maeneo tofauti wanaohitaji kuwekeza kwenye sekta ya gesi asili kujitokeza kwa wingi kwani gesi inapatikana hapa nchini ili kuwahudumia wananchi.






Related Posts