Endapo ungewasikiliza wengi nchini Ujerumani, ungefikiri ushirikishwaji wa nchi hiyo wa wahamiaji na watafuta hifadhi unakwenda vibaya. Lakini utafiti mpya wa Shiŕika la Ushiŕikiano wa Kiuchumi na Maendeleo, OECD, lenye wanachama 38 unaonyesha kuwa sivyo.
Licha ya changamoto kadhaa – kama vile elimu zaidi na mafunzo – Ujerumani inafanya kazi bora zaidi kuliko majirani zake wengi wa Ulaya linapokuja suala la kuunganisha wapya waliowasili, utafiti huo unaonyesha.
Kwa utafiti huo, mtaalam wa uhamiaji wa OECD Thomas Liebig alilinganisha data kutoka nchi kama vile Australia, Ubelgiji, Denmark, Ufaransa na Italia, na pia kutoka mataifa ya Skandinavia. Kwa mara ya kwanza, data za kina kutoka Umoja wa Ulaya pia zilitumiwa.
Ugunduzi wake: Ingawa umakini mkubwa unaelekezwa kwa waomba hifadhi na wakimbizi, uhamiaji mkubwa nchini Ujerumani unatokana na raia wa Umoja wa Ulaya wanaohama kutoka mataifa wanachama.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Liebig alisema wakimbizi wanaunda takribani mhamiaji mmoja kati ya watano waliowasili Ujerumani katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
“Idadi kubwa ya wanaowasili Ujerumani wanatoka ndani ya Umoja wa Ulaya,” alisema.
Angalizo kwenye ramani ya uhamiaji ya Ujerumani linaweka wazi hilo: Takriban asilimia 60 ya watu huja kwa sababu raia wa Umoja wa Ulaya wanaweza kupata kazi kwa urahisi hapa.
Utafiti huo pia unaweka wazi kwamba wahamiaji kwa muda mrefu wamekuwa sehemu ya jamii ya Ujerumani.
“Sisi ni nchi ya wahamiaji”
Kamishna wa ushirikishwaji wa Ujerumani Reem Alabali-Radovan, ambaye aliagiza utafiti huo, anakubaliana na mtazamo huo.
“Siku zote tumekuwa nchi ya wahamiaji na hiyo imetufanya kuwa na nguvu,” alisema. “Historia ya uhamiaji ya Ujerumani ni tofauti sana. Inajumuisha wakimbizi kutoka Vita vya Pili vya Dunia, wafanyakazi wa kigeni na wa muda, Wajerumani wa kikabila waliopewa makazi mapya, na wakimbizi kutoka Yugoslavia ya zamani na baadaye kutoka Syria na Afghanistan.”
Ushiriki wa wafanyakazi ni sifa kuu ya ushirikishwaji wenye mafanikio. Utafiti wa OECD uligundua kuwa asilima 70 ya wale wanaokuja Ujerumani wamepata ajira. Idadi hiyo, ambayo ilipungua kwa muda wakati wa janga la UVIKO-19, ni kubwa kuliko karibu katika mataifa yote ya Umoja wa Ulaya na ni rekodi kwa Ujerumani.
Matatizo ya ukosefu wa elimu ya wahamiaji
Hata hivyo bado kuna matatizo mengi: Ingawa karibu theluthi mbili ya wahamiaji wanaweza kuzungumza Kijerumani vizuri ndani ya miaka mitano baada ya kuwasili nchini, idadi hiyo inapungua kwa kiasi kikubwa miongoni mwa wale walio na elimu ndogo au wasio na elimu rasmi – huku robo tu ya waliofika wenye elimu duni wakiweza kuzungumza lugha hiyo baada ya miaka mitano.
Fursa za ajira pia ni ndogo miongoni mwa wahamiaji kama hao, zikiwa karibu asilimia 50. Kwa upande mwingine, ni Italia pekee inayowapokeawahamiaji wengi wasio na elimu rasmi.
Alabali-Radovan analiona hili kama eneo la kuboreshwa: “Mfumo wa elimu bado haujalenga kuhudumia jamii ya wahamiaji ambayo tumegeuka tangu zamani. Ndiyo maana sote tunahitaji kushirikishwa.”
Suala jingine ni ajira miongoni mwa wanawake vijana ambao wamekuja Ujerumani na angalau mtoto mmoja lakini bila mpenzi. Mnamo mwaka wa 2021, karibu asilimia 40 ya wanawake hao walikuwa wakifanya kazi kwa bidii, ikilinganishwa na asilimia 70 ya wanawake waliomo katika hali sawa na hiyo waliozaliwa nchini Ujerumani. Pengo hilo ni kubwa zaidi kuliko lilivyo katika nchi nyingine na hivi karibuni limeathiri wanawake wenye watoto wanaowasili kutoka Ukraine.
Wito wa usawa zaidi katika mjadala wa hisia
Lakini pamoja na masuala ya uhamiaji, Ujerumani haiwezi kumudu mijadala mirefu, isiyo na tija kuhusu iwapo nchi hiyo ni ya wahamiaji au la, utafiti huo unaonyesha.
“Sasa kuna zaidi ya wahamiaji milioni 14 nchini Ujerumani. Na tukiongeza wale waliozaliwa hapa kwa wazazi wahamiaji, hiyo ina maana kwamba mtu mmoja kati ya watano hapa alizaliwa nje ya nchi au alizaliwa Ujerumani na wazazi wahamiaji,” alisema Liebig ambaye ni mtaalamu wa uhamiaji.
Kamishna wa Ushirikishaji Alabali-Radovan aliongeza kuwa aliagiza utafiti huo kuleta usawa zaidi kwa kile alichokiita “mjadala wa hisia.” “Ushirikishaji unaenda vizuri zaidi kuliko inavyofikiriwa kwa ujumla, tunapoutazama kimataifa,” alisema.
Marekani nchi pekee ya OECD yenye wahamiaji zaidi
Mbali ya wahamiaji milioni 14 ambao tayari wanaishi Ujerumani, 2022 ilishuhudia kuwasili kwa raia milioni 1 wa Ukraine pamoja na waombaa hifadhi wengine 600,000.
Miongoni mwa mataifa wanachama wa OECD, ni Marekani pekee inayochukua wahamiaji zaidi kuliko Ujerumani.