Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa Temeke (TRRH) imepokea rasmi magari mawili ya kubeba
wagonjwa, ambayo yamezinduliwa na Mhe. Dorothy Kilave, Mbunge wa Jimbo
la Temeke. Ujio wa magari haya yanaenda kuboresha huduma za rufaa na za
dharura zilizopo hospitalini hapo, na kufanya idadi ya magari ya kubeba
wagonjwa kuwa matano.
Mganga
Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Joseph Kimaro, amethibitisha maboresho
haya wakati akiwasilisha taarifa fupi ya utendaji kazi na maboresho
katika hafla ya ugawaji wa magari ya kubeba wagonjwa mbele ya mgeni
rasmi, Mhe. Dorothy Kilave.
Dkt. Kimaro ameeleza mafanikio mbalimbali ya hospitali hiyo moja ikiwa
ni kununua kifaa tiba kinachoitwa laparoscopy tower, ambacho kitawezesha
hospitali kufanya upasuaji kwa njia ya tundu ndogo, hivyo kupunguza
rufaa ya wagonjwa kwenda katika hospitali za juu.
Aidha,
kupitia utendaji mzuri wa timu ya uendeshaji wa huduma za afya,
hospitali imeanza kutoa huduma za usafishaji damu (dialysis), na ndani
ya wiki kadhaa imefanya sesheni 28 kwa wagonjwa nane waliopatiwa huduma.
Kwa upande wake, Mhe. Dorothy Kilave amepongeza juhudi za hospitali
katika kuhakikisha wanaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi. Amesema
kuwa kila anapofika hospitalini hapo anakuta kuna maboresho mapya ambayo
wananchi wa Temeke wamekuwa wakiyatamani.
Mhe.
Kilave ametoa shukrani na pongezi kwa kazi nzuri inayofanywa na Mhe.
Rais kwa kusaidia na kusikiliza mahitaji ya majimbo mengi. Ameongeza
kuwa, kwa siku ya leo, tunashuhudia Jimbo la Temeke likipokea vifaa hivi
vya magari ya kubeba wagonjwa.
Aidha, maboresho na mafanikio haya yanatupa moyo kuona kuwa kweli kazi
zinafanyika. Pia, amehakikishia uongozi juu ya uwepo wa fedha
zitakazowezesha ujenzi wa gorofa sita litakalosaidia kupunguza na
kuondoa changamoto ya ufinyu wa eneo.