Kagame kuendelea kurindima Dar,Singida BS mzigoni leo

BAADA ya jana kupigwa michezo minne ya ufunguzi wa michuano ya Kombe la Kagame, Ligi hiyo itaendelea tena leo ambapo itakuwa ni zamu ya timu za kundi ‘B’, mechi zote zikipigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam.

Mchezo wa mapema utakuwa kati ya Al Hilal ya Sudan itakayocheza dhidi ya Djibouti Telecom ya Djibouti saa 12:00 jioni huku mabingwa mara tatu wa michuano hiyo, Gor Mahia ya Kenya itacheza na Red Arrows ya Zambia kuanzia saa 3:00 za usiku.

Michuano hii iliyoanza jana huku ikitarajiwa kuhitimishwa Julai 21, awali ilipangwa kufanyika Julai 20 hadi Agosti 4, ila baada ya ratiba ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kubana ikabidi kurudishwa nyuma ili kukidhi mahitaji ya timu.

Mbali na kurudishwa nyuma, ila michuano hii pia awali ilipangwa kupigwa na visiwani Zanzibar ingawa imeshindwa kufanyika na sasa itachezwa jijini Dar es Salaam pekee, huku viwanja vitakavyotumika ni vya KMC na ule wa Azam Complex Chamazi.

Michuano hii inawakilishwa na timu 12 kutoka Mataifa tofauti ya Ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati maarufu (CECAFA), zikiwa makundi tofauti ambapo kundi ‘A’ ni Coastal Union (Tanzania), Al Wadi (Sudan), JKU (Zanzibar) na Dekedaha kutokea Somalia.

Al-Hilal Omdurman ya Sudan, Gor Mahia (Kenya), Red Arrows (Zambia) na Djibouti Telecom ya Djibouti zinaunda Kundi ‘B’ huku Kundi ‘C’ likiwa na timu za SC Villa (Uganda), APR (Rwanda), Singida Black Stars (Tanzania) na Al-Merrikh ya Sudan.

Simba, Yanga na Azam FC ni miongoni mwa timu ambazo awali zilipangwa katika michuano hii japo zilijitoa kwa kile ambacho kilielezwa kubanwa na ratiba hususani baada ya kupanga kwenda nje ya nchi kwenye maandalizi ya msimu mpya ‘Pre Season’.

Kukosekana kwa vigogo hao, ni wazi michuano hii imekosa mvuto ingawa uwepo wa timu kama Gor Mahia, Singida Black Stars, Al Hilal, Red Arrows, APR, SC Villa na Al-Merrikh utaamsha morali kutokana na aina ya wachezaji wakubwa waliokuwa nao.

Meneja wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto alisema, michuano ya msimu huu itasaidia sana timu ambazo zinashiriki kujipanga vizuri kwa ajili ya msimu ujao, kwani ni sehemu ya maandalizi ya msimu ‘Pre Season’.

Kwa upande wa Ofisa Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars, Hussein Massanza alisema, licha ya timu hiyo kupangiwa kundi gumu la ‘C’, ila malengo yao ni kuleta ushindani mkubwa utakaowafanya kutwaa taji hilo kwa ukanda huu wa CECAFA.

“Kundi letu ni gumu kuliko mengine ila ni kipimo sahihi kupima ubora na daraja letu kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Bara kwani hata kocha wetu, Patrick Aussems alishauri pia tushiriki ili kupanga mbinu na kuangalia aina ya wachezaji wetu.”

Related Posts