Kikwete aliiba kura 2010, nilimnyang’anya mic…

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa amekumbushia machungu ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na kusisitiza kuwa anaamini alishinda uchaguzi huo katika nafasi ya rais lakini aliyekuwa mgombea wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alimuibia kura. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Dk. Slaa ambaye pia aliwahi kuhudumu nafasi ya balozi wa Tanzania nchini Sweden kwa miaka minne, amedai kuwa alipozunguka nchi nzima alioneshwa ushahidi wa karatasi za kura walizompigia.

Hata hivyo, mara kadhaa CCM imekana kuwahi kuiba kura kama alivyosema Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makala ambaye tarehe 4 Juni mwaka huu alisema  CCM ipo imara, haijawahi kuiba kura na kitashinda kwa kishindo katika uchaguzi ujao.

Akizungumza katika kituo cha runinga cha Clouds, Dk. Slaa amesema licha ya kukataa kumtambua Rais Kikwete wakati huo, ilimbidi afanye naye kazi kwa sababu hapakuwepo na rais mwingine.

Dk. Slaa ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa hospitali ya CCBRT, amesema amefanya kazi na Rais huyo mstaafu katika matukio mbalimbali ya harambee kwa ajili ya matibabu ya walemavu kwenye hospitali hiyo.

“Najua aliiba kura… nilishinda uchaguzi 2010 lakini waliiba. Ningekuwa na hasira na Kikwete nisingefanya naye kazi lakini lazima ufanye kazi hizo za fundraising,” amesema.

Akizungumzia alivyorejea nchini baada ya kuikacha Chadema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kukimbilia Canada, Dk. Slaa amesema baada ya kurejea Disemba mwaka huo, alishiriki harambee kwa ajili ya hospitali hiyo akiwa ameambatana na Rais Kikwete.

Amesema katika moja ya matukio ya aina hiyo, Rais Kikwete ambaye alikuwa mgeni rasmi alipopewa nafasi ya kutoa hotuba alianza kwa salamu ya ‘CCM Oyee’ ambaye ni ya kisiasa hali iliyomlazimu Dk. Slaa kumnyang’anya rais huyo mstaafu kipaza sauti (mic).

“Mara ya kwanza Kikwete alikuwa hajui mimi ni mtu wa namna wa namna. Akaanza kusema CCM oyee. Nilimnyang’anya mic nikamuambia ukitaka siasa na mimi naijua, nihakikishie hutoendeleza siasa hapa… Kikwete alirudi hakuongea tena neno la kisiasa,” amesema Dk. Slaa.

Related Posts