KTO, TaTEDO WATOA MAFUNZO YA UTENGENEZAJI MAJIKO SANIFU KWA WAKUFUNZI VYUO VYA MAENDELEO YA WANANCHI (FDC’s)

Washiriki waishukuru KTO kwa kuwezesha mafunzo hayo, waahidi kupeleka maarifa hayo kwa jamii

MAFUNZO Maalum ya utengenezaji majiko sanifu ya kupikia kwa kutumia kuni chache na gharama nafuu yanatarajiwa kuwaanufaisha wananchi kupitia wakufunzi wa ufundi kutoka vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC’s) ambao wamepewa mafunzo hayo na Taasisi za Huduma za Nishati Endelevu (TaTEDO) na kutakiwa kuyapeleka kwa jamii.

Akizungumza na Michuzi Blog Mtaalamu wa majiko sanifu na masuala ya nishati mbadala kutoka TaTEDO Gabriel Paulo amesema; Katika mafunzo hayo yaliyohusulisha wakufunzi wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC’s) kutoka maeneo mbalimbali nchini ambapo wameshirikishana kuhusiana masuala mbalimbali ya nishati safi ya kupikia pamoja na utunzaji wa mazingira.

Ameeleza kuwa katika jitihada za kumtua Mama mzigo wa kuni na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia wadau wakiwemo TaTEDO na KTO wameibea ajenda hiyo kwa kuwafikishia wananchi hususani wa vijijini na wenye kipato kidogo majiko hayo sanifu ya gharama nafuu yenye kutumia kuni chache ili kupunguza kasi ya uharibifu wa mazingira na kulinda afya ya mtumiaji.

Pia amesema, mafunzo hayo pia yatatoa fursa ya ujasiriamali kwa wakufunzi na wanufaika wa mafunzo hayo waliopo katika mazingira ya vyuo hivyo huku gharama za ujenzi wa majiko hayo yakielekezwa na TaTEDO ili wananchi waweze kumudu.

Amesema,Baada ya kupata elimu ya darasani wamehamia katika vitendo ambapo wakufunzi hao wamekuwa na uelewa kuhusiana na ufundi wa majiko sanifu ambapo jiko moja lililochaguliwa na taasisi litajengwa na likikamilika litafanyiwa majaribio.

” Tumepata wakufunzi wa vyuo ambao wana uelewa mkubwa wa ujenzi na wana uzoefu…Tunataraji mafunzo haya yatawafikia wananchi wengi zaidi kutokana na uzoefu na udadisi kutoka kwa wakufunzi hawa kutoka vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.” Amesema.

Aidha amesema, majiko hayo yanasaidia sana katika utunzaji wa mazingira kwa kuwa yanatumia kuni chache na gharama ya ujenzi wake ni rahisi kwa jamii kuweza kumudu.

“Kwa utafiti mdogo nilioufanya baadhi wa wanawake hutembea umbali mrefu kutafuta kuni takribani mara tatu kwa wiki…Jiko hili lina msaada na limepunguza changamoto hiyo kwa kuwa wanawake wanaenda kutafuta kuni mara moja kwa wiki kutokana na jiko sanifu kutumia kuni chache zaidi ambayo pia husaidia katika kuhifadhi mazingira na hata athari za kiafya pia kwa kuwa kwa kutumia jiko hili moshi haumzingili na kumuathiri mpishi.” Amefafanua.

Amesema jiko hilo banifu limekuwa msaada katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Mtwara, kambi za wakimbizi Kigoma na Masasi ambapo matokeo yake yamekuwa yakiridhisha kimazingira na afya pia.

Kwa upande wake Mkufunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Ulembwe FDC kutoka mkoani Njombe Stanford Ndola amesema kuwa mafunzo hayo ya utengenezaji majiko sanifu na utunzaji wa mazingira yamekuwa na tija kwao, taasisi wanazofanyia kazi na jamii inayowazunguka.

” Kupitia mafunzo haya tutabeba maarifa haya na kwenda kufundisha katika taasisi zetu na jamii inayozunguka vyuo vya Maendeleo ya Wananchi na tunaamini itasaidia sana katika utunzaji wa mazingira.” Amesema.

Aidha amelishukuru Shirika lisilo la Kiserikali la Karibu Tanzania Organization (KTO,) kwa kuwezesha mafunzo hayo ambayo ni chachu katika vyuo vya Maendeleo ya Wananchi hususani katika utunzaji wa mazingira na uendelevu wake pamoja na Taasisi ya Huduma za Nishati Endelevu (TaTEDO,) kwa kutoa wakaufunzi mahiri walioweza kutoa maarifa ya kutengeneza majiko sanifu ya kupikia kwa kuni chache ambayo pia yatapunguza wimbi la ukataji wa miti.
Mtaalamu wa majiko sanifu na masuala ya nishati mbadala kutoka (TaTEDO,) Gabriel Paulo akizungumza na Michuzi Blog kuhusiana na mafunzo hayo na kueleza kuwa; Katika mafunzo hayo yaliyohusulisha wakufunzi wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC’s)kutoka maeneo mbalimbali nchini ambapo wameshirikishana kuhusiana masuala mbalimbali ya nishati safi ya kupikia pamoja na utunzaji wa mazingira. Leo jijini Dar es Salaam.
 

Mkufunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Ulembwe FDC kutoka mkoani Njombe Stanford Ndola akizungumza na Michuzi Blog na kueleza  kuwa mafunzo hayo ya utengenezaji majiko sanifu na utunzaji wa mazingira yamekuwa na tija kwao, taasisi wanazofanyia kazi na jamii inayowazunguka. Leo jijini Dar es Salaam.



 

Matukio mbalimbali ya hatua za ujezi wa jiko sanifu la mfano.

Related Posts