Kucheza na njaa kulivyomkimbiza Nelly Ligi Kuu

UKITAJA mabinti warembo 10 wanaofanya vizuri katika Ligi Kuu ya Wanawake Bara, basi huwezi kumuacha mwanadada Nelly Kache anayekipiga Alliance Girls ya jijini Mwanza.

Licha ya kucheza Tanzania, lakini ndoto zake kubwa ni kusakata kabumbu Ufaransa ambako anaamini atakuza zaidi kipaji chake.

“Tanzania unapata fursa nyingi ya kuonekana. Naamini kuna mawakala mbalimbali wanafuatilia ligi hii na ndoto yangu inaweza kutimia kucheza Ufaransa siku moja,” anasema Nelly ambaye amemaliza ligi hiyo akiwa kinara wa mabao Alliance akitupia kambani matano.

Kiungo huyo mshambuliaji huu ni msimu wake wa nne kucheza Bongo akitokea katika Klabu ya MTG ya nchini kwao, Kenya kabla ya kuja Tanzania kuitumikia Fountain Gate Princess mara ya kwanza mwaka 2021.

Anasema mwaka 2020 wakati anakuja jijini Dodoma kusaini mkataba na Fountain, ikiwa ndio mara ya kwanza kufika Tanzania, kidogo apotee wakati anazunguka akiitaja kama changamoto ya kwanza kukutana nayo nchini.

“Wakati huo nakuja, hakuna ninayemjua tofauti na sasa, nilipata tabu sana nilikuwa natoka Mombasa kuja Dodoma. Nilitumia simu hadi kufika lakini kilichonichosha kuuliza njiani,” anasema.

“Kusema ukweli Watanzania wana upendo sana, mtu hawamjui lakini walikuwa wananielekeza hadi nikajihisi na mimi ni wa nchi hii, kwetu Kenya kuelekezwa tu unatoa pesa tena unaweza kuibiwa kabisa na mizigo yako.”

“Huwa sipendi kuyaweka hadharani mafanikio yangu kwa sababu sio wote watafurahia, lakini kiukweli kama soka lingekuwa halilipi basi nahisi ningeacha muda tu, riziki napata sio haba na kuna mafanikio nimeyafanya kama kuanzisha biashara kwetu Kenya,” anasema.

KWA NINI HAKAI NA TIMU MUDA MREFU?

Ni miaka minne sasa tangu atue nchini mwaka 2020 akizitumikia Fountain Gate Princess, The Tigers Queens na Alliance Girls na kote amecheza msimu mmoja kila timu.

“Ni kweli nimecheza timu tatu tofauti kwa hapa Tanzania na kila timu nimedumu kwa msimu mmoja, ni makubaliano tu baina yangu na timu ninayoichezea,” anasema Nelly.

“Huwa napenda hivyo kwa sababu pia ya kubadilisha mazingira. Mfano nimecheza Fountain ipo Dodoma, Tiger Queens Iringa na sasa Alliance yenye makao makuu yake Mwanza. Inanisaidia kufahamu sehemu mbalimbali za nchi ya Tanzania.”

Nelly anasema ukiachana na timu hiyo kufanya vibaya jambo lililomkimbiza Tiger Queens ni ukata.

“Huku Alliance kuna tofauti kidogo, Tiger kulikuwa na shida sana kuna muda hata chakula wachezaji tulikuwa tunakosa ukiingia uwanjani unachezaje ilhali hujala,” anasema.

Akizungumzia tabia ya baadhi ya mastaa wa ligi hiyo kujiweka katika mwonekano wa kiume, mchezaji huyo anasema: “Sioni sababu ya kucheza mpira na kujiweka kiume kwa sababu kadri utakavyojiweka hivyo ndio watu watakuchukulia vibaya.

“Sisi ni watoto wa kike hata tujiweke vipi (kiume) bado tunahesabiwa wanawake, ndiyo maana napenda kujiweka uhalisia wangu (ulivyo) maana kuna maisha nje ya soka. Utashindwa kuolewa kwa sababu ya mwonekano,” anasema.

“Unakuta kwenye timu, nusu ya kikosi wanajiweka kiume basi watu wakiwaona hivyo wanawachanganya na nyie ambao hamjiweki. Mbaya zaidi sipendi (baadhi ya watu) wanavyotuita majike dume. Ni neno linalonichukiza sana.”

Nelly anasema soka la Tanzania lina changamoto zake, lakini kwenye suala la pesa analiamini kwa asilimia 80 na wachezaji wanazingatiwa upande huo.

“Kenya ngumu sana kutoboa kimaisha kwa sababu utacheza tu kwa kujifurahisha tofauti na Bongo pesa ipo, ingawa posho itachelewa, lakini utapewa ndio maana wachezaji wengi wanatoka huko kuja Tanzania,” anasema.

Anasema mkwanja mkubwa aliowahi kuupata kwenye soka ni Sh2 milioni alizopewa kama ada ya usajili mwaka 2020 wakati yupo Kenya. “Nilipopata nikaanzisha biashara fulani hivi ambayo hadi sasa bado naendelea nayo. Nyingine nikampatia mama akawalipie ada wadogo zangu wawili,” anasema mchezaji huyo.

Nelly anasema anatamani kumaliza maisha ya soka ndipo aolewe na kuanzisha familia kama wanawake wengine.

“Kiukweli sipendi kuharibu malengo yangu na kuna ugumu kidogo wa kuwa na familia huku unacheza kwa sababu soka linahitaji nguvu pia. Kwa hiyo ukijifungua kuna vitu vitapungua lakini natamani nimalize soka kisha niwe na familia yangu.”

Related Posts