MAJALIWA AWAPONGEZA RAIS SAMIA NA DKT. MWINYI KWA SERA BORA SEKTA YA FEDHA.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Tawi la Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) mkoani Morogoro, Julai 09, 2024. Kushoto ni  Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Mhe. Hamza Hassan Juma, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya PBZ Arafat Haji (Picha Ofisi ya Waziri Mkuu)

……

-Asema zimekuwa msingi katika ukuaji wa sekta ya fedha.

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewapongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa sera nzuri za fedha na Uchumi ambazo zimekuwa  msingi wa ukuaji wa sekta ya fedha hususan katika kuleta suluhisho la huduma za kifedha kwa Wananchi.

Amesema kuwa kupitia Sera hizo kumekuwa na  mabadiliko makubwa  mpaka kwenye ngazi za vitongoji na kusaidia sana kusogeza huduma kwa wananchi kupitia taasisi za fedha.

Amesema hayo leo (Jumanne, Julai 09, 2024) wakati alipozindua tawi la benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) mkoani Morogoro.

Amesema kuwa uzinduzi wa benki hiyo ni mpango wa kuendeleza dhamira ya Dkt. Samia wa kuleta maendeleo ya haraka kwa Watanzania kupitia uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. “Ni azma ya Serikali ya awamu ya sita kuhakikisha kwamba huduma za kifedha zinapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu kwa kila mwananchi”

Ameongeza kuwa ufunguzi tawi hilo katika mkoa wa Morogoro utakuwa ni miongoni mwa vichocheo vya maendeleo ya kiuchumi katika kuwahudumia Wananchi.

Amesema kuwa licha ya kutoa huduma za kibenki, uwepo wa benki hiyo unatoa fursa ya kuchangia upatikanaji wa ajira kwa vijana. “Kwa upande mwingine tawi hili ni kichocheo cha shughuli za kiuchumi katika eneo hili kujenga msingi imara wa maendeleo endelevu na ustawi wa jamii yetu.”

“Hii ni kutokana na ukweli kwamba huduma za kibenki ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi, uzinduzi wa tawi hili ni ishara ya maendeleo na uwekezaji katika sekta ya kifedha hii ni fursa muhimu kwa Wana-Morogoro kuongeza uwezo wao wa kupata mitaji kwa ajili ya shughuli zao”

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Morogoro kutumia fursa ya uwepo wa benki hiyo kuchangamkia huduma zinazotolewa ikiwemo mikopo ambayo itawawezesha kupata fedha na kuendesha shughuli zao za kiuchumi.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Hamza Hassan Juma Amesema kuwa benki hiyo itasaidia kuwaunganisha wakulima wa mpunga waliopo Morogoro na ndugu zao waliopo Zanzibar kwani “Wakulima wa mpunga hapa Morogoro ni Wazanzibar hivyo benki hii itasaidia kuwaunganisha na ndugu zao wengi waliopo Zanzibar”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya PBZ Arafat Haji amesema kuwa uzinduzi wa benki hiyo katika mkoa wa Morogoro utasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha biashara kati ya Tanzania Bara na Zanzibar hada ikizingatiwa mkoa wa Morogoro ni mzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo.

“Kwasasa wateja wetu hawatakuwa na adha ya kusafiri kwenda Dodoma, Dar es Salaam au Zanzibar kufuata huduma za kibenki, hapa Morogoro ni kiunganishi kati ya Dar es Salaam na Dodoma”

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifungua kitambaa kuashiria uzinduzi wa Tawi la Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) mkoani Morogoro, Julai 09, 2024. Kushoto ni  Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Mhe. Hamza Hassan Juma, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya PBZ Arafat Haji (Picha Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Tawi la Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) mkoani Morogoro, Julai 09, 2024. Kushoto ni  Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Mhe. Hamza Hassan Juma, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya PBZ Arafat Haji (Picha Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipewa maelezo na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya PBZ Arafat Haji kabla ya uzinduzi wa Tawi la Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) mkoani Morogoro, Julai 09, 2024. (Picha Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua jengo la Tawi la Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) mkoani Morogoro kabla ya uzinduzi wake, Julai 09, 2024. (Picha Ofisi ya Waziri Mkuu)

Related Posts