BAADA ya dili la kumpata Yusuf Kagoma ili kuongeza nguvu eneo la kiungo kushindikana na nyota huyo kutambulishwa Simba jana, Yanga imejibu mapigo kwa kushusha kiungo mwingine atakayecheza nafasi hiyo.
Ipo hivi; Yanga ilikuwa ya kwanza kumfuata Kagoma aliyeitumikia Singida Fountain Gate msimu uliopita ili kumpa mkataba, lakini wakati ikiendelea kujadili juu ya ishu ya maslahi, Simba ikaingilia dili hilo na kumaliza mchezo mapema.
Baada ya Simba kukamilisha kila kitu jana ikamtambulisha na kuiacha Yanga ikihamishia nguvu sehemu nyingine.
Hivi sasa inaelezwa kwamba Yanga haijakaa kinyonge kwani ilipoona mambo magumu kwa Kagoma, ikamvutia waya Aziz Andambwile na ipo katika hatua nzuri ya kumalizana. Kumbuka nyota hao wote msimu uliopita walikuwa Singida Fountain Gate wakicheza kikosi cha kwanza.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Singida Fountain Gate kimeliambia Mwanaspoti kuwa ni kweli kuna mazungumzo kati yao na Yanga kwa ajili ya kiungo huyo. “Yanga wametuma ofa na mazungumzo baina yetu na wao yanaendelea, yapo kwenye hatua nzuri na muda wowote mambo yakienda sawa atatambulishwa kama mchezaji wao,” kilisema chanzo hicho.
“Tupo Dar es Salaam sambamba na mchezaji kwa ajili ya kukamilisha dili hilo. Uwezekano ni mkubwa wa kumuuza kuliko kubaki Singida Fountain Gate hivyo mtarajie lolote.” Wakati huohuo, Yanga imekiri kuwa na uhitaji wa kiungo mkabaji ambaye atasaidiana na Khalid Aucho ukiondoa Jonas Mkude ambaye pia anatakiwa kuwa na mshindani wake.
“Kati ya sehemu ambazo tunahitaji kuboresha kwa ajili ya msimu ujao ipo nafasi ya kiungo mkabaji. Ndiyo maana wamekuwa wakitajwa wachezaji wengi wanaocheza eneo hilo. Mambo yakiwa tayari kila mmoja atafahamu ni kiungo gani anasajiliwa,” kilisema chanzo kutoka Yanga.
“Ukiangalia ndani ya Yanga ukimuondoa Aucho, kuna Jonas Mkude, tulikuwa na Zawadi Mauya ambaye tayari ameondoka kikosini baada ya mkataba wake kumalizika, hivyo benchi la ufundi limeona kuna haja ya kitu kifanyike kulingana na matakwa yao.”
Chanzo hicho kilisema dirisha la usajili linaruhusu kufanya wanachofanya huku kikidai bado wanasajili na watakapomaliza watasema.
Kiliongeza kuwa hawataki kufanya makosa kwa kujaza wachezaji wa kigeni eneo moja halafu hawatumiki, hivyo wameona ni bora kusajili mzawa ili kulinda idadi ya mastaa wa kigeni ambao watasajiliwa kwa nafasi nyingine.
Andambwile alijiunga na Singida Fountain Gate 2022-2023 akitokea Mbeya City na alikuwa akicheza sambamba na Kagoma. Bado ana mkataba wa mwaka mmoja hivyo hataondoka bure.
Endapo dili la kiungo huyo litakamilika atakuwa ni mchezaji mwingine mpya wa Yanga baada ya kutambulishwa Clatous Chama, Prince Dube, Chadrack Boka na Khomeiny Aboubakar.
Jana mastaa wote wa Yanga waliingia kambini Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza ‘pre-season’.
Kabla ya kuingia walipimwa afya ambapo jioni wakaanza mazoezi ya gym huku ratiba zingine zikitarajiwa kuendelea leo.