Moscow, Urusi. Mashambulizi ya Ukraine kwenye eneo la mpaka wa Urusi la Belgorod yamewaua watu wanne ndani ya saa 24 zilizopita.
Vyacheslav Gladkov ambaye ni Gavana wa eneo hilo amethibitisha leo Jumanne, Julai 9, 2024.
Aidha, akinukuliwa na AFP, Meya wa Belgorod, mji mkuu wa eneo hilo, Valentin Demidov amesema hapo awali vikosi vya Ukraine vilianzisha mashambulizi ya usiku katika eneo hilo lote.
“Imekuwa shida sana ni saa 24 ngumu kwa mkoa wa Belgorod. Watu wanne wamekufa, 20 wamejeruhiwa, 17 wamesalia katika vituo vya matibabu, wawili kati yao katika hali mbaya.
“Vikosi vya wanajeshi vya Ukraine vinaendelea kushambulia makazi ya Mkoa wa Belgorod,” Demidov amejulisha.
Hata hivyo maofisa wa Russia wameripoti mashambulizi katika mikoa mingine ya magharibi, ikiwa ni pamoja na Kursk, Voronezh, Volgograd, Rostov na Astrakhan.
Inaelezwa shambulio hilo limetokea baada ya Russia kushambulia Ukraine Jumatatu ambapo imewaua zaidi ya watu 30.
Taarifa zinasema takriban watu 37 waliuawa, wakiwemo watoto watatu, huku zaidi ya watu 170 wakijeruhiwa.
“Mashambulizi hayo yaliharibu karibu majengo 100, zikiwemo shule na hospitali,” aliongeza Zelensky.
Urusi yadai kuharibu ndege 38 za Ukraine
Katika hatua nyingine Wizara ya ulinzi ya Russia imesema leo Jumanne vikosi vyake vimeharibu ndege 38 za Ukraine usiku kucha katika maeneo karibu na mpaka.
“Mifumo ya ulinzi wa anga iliyokuwa zamu iliharibu na kunasa UAV tatu katika eneo la Belgorod, saba katika eneo la Kursk, mbili katika eneo la Voronezh, 21 katika eneo la Rostov na UAV tano katika eneo la Astrakhan,” imesema taarifa ya wizara.
Gavana wa Astrakhan, Igor Babushkin amesema Ukraine ilianzisha jaribio la kushambulia kwa kutumia ndege zisizo na rubani Kaskazini mwa eneo hilo, na kuongeza kuwa shambulio hilo limefanikiwa kuzuiwa.
Pande zote mbili zimetumia ndege zisizo na rubani, ikiwa ni pamoja na meli kubwa ya masafa ya kilomita kwa kiasi kikubwa katika mzozo huo, ulioanza Februari 2022.
Rais wa Urusi, Vladimir Putin alianzisha mashambulizi mapya ya ardhini katika eneo la Kaskazini-Mashariki mwa Ukraine la Kharkiv Mei mwaka huu, katika operesheni ya kuvirudisha nyuma vikosi vya Ukraine ili kulinda mpaka wake eneo la Belgorod dhidi ya mashambulizi ya makombora.
Nchi hizo mbili zimekuwa katika mapigano hususani katika eneo la mpakani tangu uvamizi wa Urusi Februari 24, 2022.