Waziri Mkuu Modi alitoa matamshi hayo kwenye televisheni, alipokutana na Rais Putin katika Ikulu ya Kremlin, kwenye ziara yake nchini Urusi.
“Mheshimiwa, vita, mapambano, au mashambulizi ya kigaidi, kila mtu anayeamini katika ubinadamu anahisi uchungu watu wanapopoteza maisha. Na hata huko, watoto wasio na hatia wanapouawa, kuna mtu anayewaona wanakufa, moyo unauma, ni maumivu yasiyovumilika, na tulijadiliana katika muktadha huu pia.”
Waziri Mkuu Narendra Modi anazuru Moscow kwa mara ya kwanza tangu taifa hilo lilipomvamia jirani yake Ukraine mapema mwaka 2022. Na ziara yake imetiwa kiwingu na shambulizi kwenye hospitali moja kubwa ya watoto mjini Kyiv, ambalo mamlaka za Ukraine zinasema lilifanywa na Urusi.
India na Urusi wana mahusiano ya muda mrefu
Urusi hata hivyo, imekana, na kusema tu kwamba ni mifumo ya Ukraine ya kujilinda na makombora ya angani ndiyo iliyosababisha janga hilo, ambapo karibu watu 140 waliuawa.
Soma pia: Watu zaidi ya 30 wauwawa katika shambulizi la Urusi, Ukraine
Modi amemsisitizia Putin kama kiongozi mwenzake na rafiki yake kwamba, suluhu inaweza kupatikana kwa mazungumzo na sio kwenye uwanja wa vita.
Putin kwa upande wake alizungumzia zaidi uhusiano mzuri wa kimkakati baina ya mataifa hayo na kumshukuru Modi kwa juhudi zake katika kusaka suluhu ya amani kuelekea vita hivyo.
Alimkaribisha Modi kwenye ikulu ya Kremlin kwa ajili ya mazungumzo kuhusiana na kuimarisha zaidi uhusiano wa mataifa yao, siku moja baada ya Marekani kusema imeanza kutilia mashaka ushirika wake na India, kutokana na urafiki huu kati ya Moscow na New Delhi.
Soma pia: Waziri Mkuu wa India Modi aelekea Moscow, Vienna wiki ijayo
Wamekubaliana pia kuimarisha ushirikiano katika sekta kuanzia nguvu za nyuklia, ujenzi wa meli na kushughulikia changamoto ya malipo.
India, imeendelea kuwa mshirika muhimu kwa Urusi iliyoelemewa na vikwazo vya magharibi, wakati ikiangazia ushiriki wa kibiashara kwenye maeneo mengine, na kuachana na magharibi, lakini pia ikitaka kuwaonyesha kwamba juhudi zao za kuitenga hazikufua dafu.
Umoja wa Mataifa wathibitisha Urusi ilishambulia hospitali mjini Kyiv
Huku hayo yakiendelea, matokeo ya uchunguzi wa awali uliofanywa na ofisi ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa yameonyesha kwamba kombora la Urusi chama Kh-101 ndilo lililoshambulia hospitali hiyo ya watoto ya mjini Kyiv.
Mkuu wa Ujumbe wa umoja huo unaofuatilia haki za binadamu nchini Ukraine Danielle Bell amesema hayo hii leo na kuongeza kuwa wataalamu wamefikia hitimisho hilo baada ya kuchunguza picha za vidio na kwenda kushuhudia uharibifu kwenye eneo hilo.
Bell, aliliita shambulizi hilo kuwa ni baya kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu Urusi ilipoivamia Ukraine na kusema idadi ya vifo ingekuwa kubwa zaidi kama wafanyakazi wa afya wasingewahamishia mafichoni wagonjwa muda mfupi kabla ya shambulizi hilo.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Francis naye amesema amesikitishwa sana na shambulizi hilo, na kuelezea mashaka yake kuhusiana na kuongezeka kwa mzozo huo.