Gilbert Msuta Meneja wa Sehemu ya Uhaulishaji wa Teknolojia kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) ameeleza kuwa moja ya tafiti kubwa ambayo taasisi imeifanya kwa miaka mingi na ambayo kwa kiasi kikubwa imewafikia wadau wengi ni teknolojia ya ng’ombe aina ya Mpwapwa ambae amezalishwa ili kumuwezesha mfugaji mwenye rasilimali chache kuwa na uzalishaji wenye tija hasa wa nyama na maziwa.
Kauli hiyo ameitoa kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwl. Julius Nyerere jijini Dar es salaam ndani ya banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi yakiwa na kauli mbiu isemayo “Tanzania: Mahali Sahihi Pa Biashara Na Uwekezaji”
Msuta ameendelea kueleza kuwa ng’ombe huyo ambae ana mchanganyiko wa ng’ombe wa damu ya ng’ombe wa mabara mengine ikiwemo damu ya ng’ombe aina ya boran na ng’ombe wa asili wa Tanzania kwanza lengo la kumuwezesha ng’ombe huyo kuwa na vinasaba vitakavyomfanya azalishe maziwa mengi, awe na nyama nyingi lakini pia awe na uwezo wa kustahimili magonjwa.
“Kwa bahati nzuri ng’ombe huyu ameonekana kufanya vizuri kwenye maeneo yenye nyanda kame na wafugaji wengi wa maeneo ya Kiteto, Dodoma, Singida na maeneo mengine mengi wamemchukua na wananufaika nae” alisema Msuta.
Pamoja na hayo Msuta amaeeleza kuwa kwa upande wa mbuzi tafiti zimefanyika na kuwezesha kupata mbuzi wa maziwa kwenye kituo cha TALIRI Tanga ambao wameonekana kufanya vizuri sana katika ukanda wa Mashariki, lakini pia uzalishaji wa mbuzi chotara wa nyama umefanyika na kupata mbuzi mwenye mchanganyiko wa damu ya asili na damu ya boer ambapo vina saba vya boer vinampa uwezo wa kuzalisha nyama kwa wingi huku damu ya asili ikimpa uwezo wa kustahimili magonjwa.
Aidha, Msuta ameeleza kuwa mbuzi hao wanafaida mbalimbali ikiwemo kutougua kila wakati, kukuwa haraka na hivyo mfugaji anaweza kuwapeleka sokoni mapema zaidi ya mbuzi wa kawaida.