BENKI ya NMB imefanya mazungumzo na wanachama wa Chemba ya Wanawake Wafanya Biashara Tanzania (TWCC), wanaoshiriki Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara, kuwaonesha fursa na masuluhisho ya kifedha yanayoweza kuchangia ustawi na kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
TWCC wanashiriki Maonesho hayo maarufu kama Sabasaba, jukwaa inayatumia kuuza na kunadi bidhaa mbalimbali zikiwemo za usindikaji, ushonaji, vipodozi na urembo, afya na tiba, tiba asilia, nk, ambako NMB imewatembelea na kuwaambia inatambua na kuthamini juhudi zao katika kuinua biashara na kukuza uchumi.
Akizungumza na wanawake hao, Katibu wa Kampuni ya Benki ya NMB, Mwantumu Salimu alisema kwa kutambua, kuthamini mchango wa kukuza uchumi wa wanawake, benki hiyo itaendelea kushirikiana na kusimama nao pamoja kwa kuwapa masuluhisho rafiki ya kifedha ili kusaidia kukua kwao kiuchumi.
“Tunatambua juhudi zenu wanawake Wafanyabiashara, mmekuwa mfano bora kwa wanawake wengi sana hapa nchini, mmekuwa hamasa kubwa pia kwa mabinti wadogo katika kujiamini na kujituma zaidi katika kazi, biashara, masomo na shuguli zingine.
“Juhudi zenu zisizo na kikomo, uweledi wenu katika kazi na uaminifu wenu wa hali ya juu, umekuwa nguzo katika kuwawezesha wanawake kwenye biashara mbalimbali na TCWW imekuwa ni kielelezo tosha kwa maendeleo makubwa tunayoona leo,” alisema Mwantumu.
Aliwaeleza kwamba, Benki ya NMB wapo katika maoenesho hayo, hivyo kuwataka kutembelea banda lao kwa ajili ya kupata huduma zote za kibenki, ikiwemo elimu ya fedha, mikopo na bima mbalimbali zikiwemo za machinga kwa ajili ya biashara zao, kupitia wataalam na kwamba watakaofika hapo watanufaika sana.
“Naomba niwakumbushe kuhusu fursa mbalimbali za mikopo, elimu ya fedha zilizopo NMB, ambazo ni muhimu sana kwenu nyie wajasiriamali, ikiwemo huduma rafiki ya Jukwaa la Mwanamke Jasiri, ambalo ni maalum kwa ajili ya wanawake, lililotengenezwa ili kutoa fursa mbalimbali za kuimarika kiuchumi.
“Pia, tunazo akaunti kama NMB Jiwekee, NMB Pesa, NMB Kikundi na nyinginezo ambazo zinatoa fursa ya kuunganishwa moja kwa moja katika huduma ya NMB Mkononi, inayomahakikishia mteja kukopa kuanzia Sh. 1,000 hadi Sh. milioni moja bila dhamana wala kutembelea tawi letu,” alibainisha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Mwajuma Hamza, aliishukuru NMB kwa kuonesha kuthamini jitihada za wanachama wake, ambao ni wanufaika wa muda mrefu wa huduma za benki hiyo, wengi wao wakiwa na akaunti, mikopo na hata bima zitolewazo na taasisi hiyo.
“Kipekee kabisa kwa niaba ya Bodi ya TWCC, kwa niaba ya Wanawake Wafanya Biashara Tanzania, tunaishukuru NMB kwa kuendelea kuwa na sisi katika ustawi wetu kiuchumi kila wakati kwa kuwasapoti wanachama wetu kwa ukaribu sana,” alisema Mwajuma.
Aliwataka wanachama wa TWCC kuhakikisha wanatumia fursa zilizoletwa na ujio wa Mwantumu katika Banda lao, kwa kuchangamkia fursa za elimu ya fedha, mikopo na bima wanazotoa, ambazo zinatoa mchango mkubwa katika kuharakisha ukuaji wao kiuchumi kupitia biashara zao.
Mmoja wa wanachama wa TWCC, aliyejitambulisha kwa jina la Janeth Munisi, alisema yeye ni mmoja wa wanufaika wa mikopo inayotolewa na NMB kwa wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa na kwamba kupitia benki hiyo, ameimarika kiuchumi na kumfanya kuajiri wanawake wengine.
“Mimi ni mfanyabiashara na mwanachama wa TWCC, niko hapa kuonesha bidhaa zetu za usindikaji. NMB ni bengi iliyonitoa mbali na ina mchango mkubwa katika hatua zangu za maendeleo, nimekopa mara nyingi, nimeshiriki semina na makongamano, pamoja na klabu za biashara za NMB,” alisema Janeth.