MAKALA ya 45 ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame yanaanza kutimua leo jijini Dar es Salaam, katika ardhi ambayo mashindano hayo yalianzia.
Mashindano hayo yalianza 1974 Dar es Salaam, hivyo kufanyika tena mwaka huu katika ardhi hii ni sawa na mtoto kurudi nyumbani.
Katika makala 44 zilizopita mashindano hayo yalifanyika mara 14 katika ardhi ya Tanzania na mara 13 ni Dar es Salaam.
Mwaka huu ni mara ya 15 katika mara zote hizo. Ni mara moja tu, mwaka 2005, Dar es Salaam haikuwa mwenyeji. Miji iliyohusika ilikuwa Mwanza na Arusha.
Cha kusikitisha mashindano yamerudi nyumbani Dar es Salaam, lakini hakuna hata timu moja ya Dar es Salaam inayoshiriki.
Waanzilishi wa mashindano na mabingwa wa kihistoria, Simba SC hawamo kwenye mashindano. Watani wao, Yanga SC ambao ndiyo wahusika wakuu kwa sababu ndiyo mabingwa wa Tanzania, hawamo kwenye mashindano.
Azam FC kama waalikwa nao hawamo kwenye mashindano. Basi angalau zingekuwepo timu zingine kutoka Dar es Salaam kama KMC au JKT Tanzania ziuheshimishe mji, lakini nazo hazimo.
Hii inakuwa mara ya kwanza kwa mashindano hayo kufanyika jijini Dar es Salaam bila timu yoyote ya Dar es Salaam.
Makala ifuatayo inakuletea mchango wa Dar es Salaam katika kufanyika kwa mashindano hayo tangu yaanze.
1. DAR ES SALAAM MWENYEJI WA KIHISTORIA
Dar es Salaam iliandaa mashindano ya kwanza ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1974 na kushuhudia watoto wa nyumbani, Simba SC wakitwaa ubingwa.
Huo ulikuwa mwanzo wa historia kubwa inayofikisha miaka 50 sasa na kushuhudia Dar es Salaam ikiendelea kuyalea mashindano hayo kama mama anavyomlea mwanaye pekee.
Makala ya mwaka huu ambayo ni ya 45 kwa jumla yatakuwa ya 15 kuandaliwa Tanzania na ya 14 kuandaliwa Dar es Salaam.
Jedwali lifuatalo linaonyesha miaka ambayo Dar es Salaam iliandaa mashindano hayo. Zaidi tu ya kuandaa, Dar es Salaam ndio mji pekee kuandaa mashindano hayo mara mbili mfululizo tena sio safari moja.
Dar es Salaam imeandaa mashindano haya mara mbili mfululizo katika safari nne tofauti na kuufanya mji huo kuwa siyo tu umeandaa mara nyingi bali mfululizo mfululizo.
Mwaka 2016 na 2017, pamoja na 2022 na 2023 mashindano hayakufanyika. Mwaka huu Dar es Salaam itaandaa mashindano haya kwa mara ya 14, ikiwa pia ni safari ya tano kuandaa mfululizo.
Wakati Dar es Salaam ikiwa imeandaa mashindano hayo mara 14, mji unaoikaribia haujafika hata nusu yake.
Miji inayoikaribia Dar es Salaam ni Kampala (Uganda) na Kigali (Rwanda) ambayo umeandaa mara sita kila mmoja, ikifuatiwa na Khartoum (Sudan) na Zanzibar (Zanzibar) ambayo imeandaa mara tano kila mmoja.
Unaweza kuona ni namna gani Dar es Salaam imeyabeba mashindano haya kwa miaka na mikaka.
DAR ES SALAAM VS MIJI MINGINE UENYEJI
Dar es Salaam (Tanzania) imefanyika mara 14: 1974, 1977, 1986 (na Mwanza), 1991 (na Tanga), 1995, 1996, 2006 (na Morogoro), 2008, 2011, 2012, 2015, 2018, 2021, 2024; Kampala (Uganda) mara sita 1976, 1978, 1987, 1993, 1999, 2003;
Kigali (Rwanda) mara tano 2000, 2004, 2007, 2010, 2014, 2019; Zanzibar mara tano 1975, 1983, 1992, 1998, 2002 na Khartoum (Sudan) mara tano 1985, 1988, 1994, 2009, 2013.
2. DAR ES SALAAM NA MAKOMBE
Japo Nairobi ndiyo mji uliobeba kombe hili mara nyingi ukifuatiwa na Dar es Salaam, lakini hata hivyo Dar es Salaam inaongoza kwa kuwa na timu iliyobeba mara nyingi zaidi kombe hili. Simba SC kutoka Dar es Salaam Tanzania, ndiyo mabingwa wa kihistoria wa mashindano haya wakibeba ubingwa mara sita.
Kwa ujumla ni timu 16 pekee ambazo zimewahi kushinda taji hili katika historia yake, orodha inayoongozwa na mwana Dar es Salaam, Simba SC.
3. DAR ES SALAAM NA FAINALI
Zaidi ya kuyaandaa, Dar es Salaam pia imeyatawala mashindano haya kwa kuhusika na fainali nyingi zaidi. Tanzania kama nchi inaongoza kwa vilabu vyake kufika fainali nyingi (26), katika hizo ni mara mbili tu ambapo Dar es Salaam haikuwa sehemu ya fainali.
Mwaka 1989 pale Coastal Union ya Tanga ilipofika fainali na kupoteza 3-0 kwa Kenya Breweries (sasa Tusker FC) mjini Mombasa Kenya, na mwaka 2006 ambapo Moro United ya Morogoro ilifika fainali mjini Dar es Salaam na kupoteza 2-1 dhidi ya Police ya Kenya.Ama kwa hakika Dar es Salaam ina historia kubwa sana na mashindano haya na itoshe tu kusema kwamba jiji hili ndiyo makao makuu ya Kombe la Kagame. Hata hivyo kukosekana kwa timu hata moja ya Dar es Salaam ni kasoro na dosari kubwa sana kwa mashindano yam waka huu.
Matarajio ni kwamba safari nyingine mashindano hayo yakirudi kwenye ardhi ya Dar es Salaam, wahusika wajipange kuhakikisha hali hii haijirudii. Siyo dhambi kukosekana kwa timu za Dar es Salaam kwenye mashindano haya, hata kama yanafanyika Dar es Salaam, lakini ni jambo jema zaidi zikawepo kwa sababu hakuna msiba au sherehe isiyo na mwenyewe.