MOJAWAPO wa maswali magumu kwa sasa ni kujua nani ataanza katika kikosi cha kwanza cha Yanga kati ya Pacome, Maxi, Aziz Kİ, Dube na Chama. Wote wanaonekana kuwa wachezaji bora. Wote wana sifa za kuanza kwenye kikosi cha kwanza.
Yanga wameendelea kuimarika kila kukicha. Yanga wamezidi kuwa bora. Inaonekana ni kama wamesajili wachezaji wengi bora wanaocheza kwenye eneo moja. Ungepewa nafasi ya Kocha Gamondi nani angeanza?
Kila mtu atakuwa na mtazamo wake. Kila mtu atakuwa na maoni yake. Khalid Uacho amekuwa roho ya timu. Aucho amefanikiwa kutengeneza shepu imara ya Yanga pale katikati. Pamoja na ubora wake wote, lakini haiondoi ukweli kuwa ameanza kuchoka.
Aucho umri nao taratibu umeanza kumtupa mkono. Yanga wanahitaji kucheza na watu wawili kama Aucho pale kati kwenye baadhi ya mechi. Aucho asitegemewe sana, ni lazima awekewe na msaidizi wa ukweli.
Msimu uliopita Maxi Nzengeli na Mudathir Yahya kwa kiasi kikubwa walimpa usaidizi mzuri. Mudathir alikwenda mbali sana na kuanza kuzalisha mabao. Ulikuwa ni wakati mzuri sana kwake. Kama ataongezewa pacha mwingine wa maana, maana yake Maxi, Chama, Aziz KI, Pacome na Dube hawawezi kuanza kwenye kikosi kimoja.
Kwa kutazama ubora, historia na mahitaji ya sasa Pacome anaweza kupata shida. Bado ni mgeni wa ligi yetu. Bado anazidiwa namba na wachezaji wengine wote niliowataja hapo juu.
Ni rahisi sana kuanza na Chama kwa sababu ameweka alama kubwa kwenye soka letu akiwa na Simba. Ni rahisi kuanza na Aziz KI kwa sababu alikuwa na msimu bora sana 2023/2024. Ni rahisi kuanza na Nzengeli kwa sababu ana uwezo wa kubaka pengine kuliko mchezaji mwingine yeyote kati ya hao niliowataja hapo awali.
Tofauti kubwa ya Pacome na Chama ni kasi. Pacome ana mwendo sana. Hana muda wa kupoteza. Kuna muda ni kama umeme huku akiacha watu msuli umewavutika. Chenga na jicho lake na pasi za mwisho ndiyo silaha yake kubwa. Sidhani kama tuna mchezaji wa aina yake kwenye ligi yetu.
Jambo moja ambalo nadhani Pacome anatakiwa kuimarika ni kuanza kufunga. Pacome alitakiwa kumaliza walau na mabao 10. Huenda ugeni wa ligi. Huenda majeraha aliyopata kuna namna yalipunguza ubora wake.
Wachezaji wote anaotakiwa kugombea nao nafasi wanafunga zaidi kuliko yeye. Wachezaji wote anaoshindana nao kwenye nafasi moja wana pasi nyingi za mwisho kuliko yeye.
Bado Pacome pamoja na burudani anayotoa, anapaswa kuongeza idadi ya mabao. Maxi Nzengeli, Clatous Chota Chama na Aziz KI hilo ndilo eneo pekee wanalomzidi kwa mbali.
Ukiambiwa kwa maoni yako utaje wachezaji watatu watakaoanza pale Yanga kwenye eneo ya Ushambuliaji utaanza na nani? Binafsi ni Chama, Aziz Kİ na Maxi kwenye mechi nyingi.
Pacome ana nafasi ya kunionyesha tena utofauti uwanjani. Ni fundi kweli mpira ukiwa mguuni. Hakamatiki kirahisi, lakini hakupi mabao mengi. Utapenda kasi yake. Ni mchezaji wa mwendokasi lakini bado sijaona sana pası zake za mwisho za uzalishaji wa mabao.
Natamani kumuona msimu huu akileta utofauti. Natamani kuona mabao mengi kwenye miguu yake. Ni msimu mmoja tu akiwa na Yanga, lakini Maxi ni mojawapo wa usajili bora kwa Yanga msimu uliopita. Ni mwendo wa kuchomekea na kuzichomeka. Huyu ni kiungo mshambuliaji au winga anayeweza kufanya kazi zote.
Maxi hata ukimpeleka Manzese ana uwezo wa kuwadhibiti vibaka. Maxi ana nguvu, akili, mwendo na maarifa sana uwanjani.
Hata akishushwa chini kwa Aucho, bado Maxi anakupa na mabao pia. Sio mburudishaji sana lakini kazi inaonekana. Ni mtu mgumu. Ni mtu katili sana akiwa na mpira uwanjani, lakini ana sura ya huruma. Hakuna wa kumuweka benchi mtu wa aina hii. Anacheza kwenye nafasi zaidi ya moja uwanjani kwa ubora uleule.
Ni wachezaji wachache sana wanakupa mchango wa Maxi dimbani. Ukipewa Maxi, Chama, Pacome na Aziz KI nani atakwenda benchi? Swali zito lenye mtazamo tofauti. Uzuri wa mchezo wa mpira wa miguu ni wa maoni. Sio lazima wote mfanane.
Kuna wachezaji wachache sana wa idara ya ushambuliaji wamekuwa wakabaji. Washambuliaji mara nyingi sana wao wanaweza kufunga. Timu ikipoteza mpira, wengi wanarudi wanatembea. Maxi ni tofauti. Akiwa na mpira mguuni anawaza kufunga, ukipotea anarudi kukaba. Hatoki mtu. Anakamba hadi kivuli na jezi kachomekea.
Hawa ndiyo wachezaji wanaoishi zama zote. Mpira wa sasa unamtaka mchezaji kama Maxi. Mchezaji anayeweza kukupa vitu vingi uwanjani. Kwa sasa hakuna wa kumuweka benchi pale Yanga. Labda ashuke kiwango. Lakini lingine labda aingie kwenye ugomvi na kocha.
Baada ya kusuasua msimu wa kwanza, Aziz KI amezaliwa upya. Sio yule tena. İdadi ya mabao aliyofunga msimu uliomalizika ni dalili tosha kuwa alistahili kutangazwa alfajiri na watu wakamsubiri. Kama unamkumbuka vyema, Aziz KI alitangazwa rasmi Yanga majira ya saa tisa alfajiri na Wananchi walikesha kusubiri usajili wake. Alikuwa na msimu mzuri sana ndani ya kimataifa.
Mfungaji bora wa ligi yetu na huenda akawa mchezaji bora wa msimu. Hakuna namna unaweza kumuweka benchi mbele ya Chama, Pacome Maxi. Hapa ndipo ugumu unapokuja. Ukipewa Chama, Pacome na Maxi nani anaanzia benchi? Kazini kwa Gamondi kuna kazi msimu ujao.
Aziz KI ni mojawapo kati ya wachezaji wenye nguvu sana. Ni moja pia ya wachezaji wenye ujuzi wa mipira ya kutenga. Ligi yetu haina mafundi wengi wa mipira ya adhabu ndogo. Walau kwa Aziz KI unaweza kuweka imani. Akipiga mashuti mara tatu anaweza kukupa bao. Ni mchezaji mdogo mwenye uwezo mkubwa sana. Moja kati ya vitu walivyofanikiwa Yanga ni kuishi naye kama familia. Aziz KI ni mtoto wa mama. Ni wale vijana ambao bado mama ana nguvu za kumuamlia uelekeo. Mama ndiye bosi wa Aziz KI. Kama Yanga watafanikiwa kumbakisha watakuwa wamebakisha jembe. Ndoto ya Yanga ya kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika inahitaji wachezaji wa aina hii.
Ndoto ya Tanzania kuwa na ligi bora Afrika, tunahitaji wachezaji wenye ubora wa Aziz KI. Twende mbele, turudi nyuma. Kazini kwa kocha Gamondi kuna kazi sana msimu ujao.