Ukisoma vyuo hivi ajira nje nje

Kama kuna majanga yanayolisibu Taifa letu kwa sasa ni pamoja na uhaba mkubwa wa ajira.

Idadi kubwa ya wahitimu katika ngazi mbalimbali wanajikuta mitaani, huku ajira rasmi zikitajwa kuwa msamiati mgeni.

Kitaifa, takwimu zinaonyesha hadi kufikia 2021, watu waliokuwa kwenye ajira walikuwa milioni 23.5. Hata hivyo, wakati wengi wakikosa ajira, wachache wanaobahatika wanatajwa kukosa weledi kazini.

Hata hivyo, baadhi ya wadau wanasema vyuo vya kada ya kati vinaweza kuwa suluhu ya tatizo la ajira nchini.

Inaelezwa kuwa vyuo hivi kwa muundo wake wa kimafunzo, vinaweza kuzalisha wataalamu mahiri kwenye fani mbalimbali ambao watakwenda kuongeza uzalishaji katika maeneo mbalimbali hasa kwa mrengo wa kujiajiri.

Maeneo ya uzalishaji ni pamoja katika kuongeza tija kwenye kilimo kwa kuwezesha mnyororo wa thamani kwa mazao yanayolimwa nchini na kutengeneza bidhaa ambazo hivi sasa zinaagizwa kutoka nje ya nchi.

Hata hivyo, baadhi ya vyuo vya kati vimejibadili na kuwa vyuo vikuu huku moja ya sababu ya kufanya hivyo ikielezwa kuwa ni kukosekana kwa wanafunzi jambo lililochangiwa na mtazamo hasi wa elimu iliyokuwa ikitolewa katika vyuo hivyo.

Juni 2, 2023, Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye alisema uamuzi wa kubaduili vyuo vya kati kuwa vyuo vikuu, umechangia kushusha kiwango cha ubora wa rasilimali watu na kusababisha vijana wengi wasomi wasiokuwa na ajira.

Miongoni mwa vyuo vya kati vilivyotamba na kupika wataalamu wengi zamani ni pamoja na IDM Mzumbe, kilichosifika kwa kutoa wahitimu mahiri kwenye fani za uongozi, uhasibu na fedha.

Kingine ni Chuo cha Ushirika Moshi, kilichokuwa kikitoa wahitimu mahiri katika sekta ya ushirika. Vyuo hivi na vinginevyo kwa sasa vimegeuzwa kuwa vyuo vikuu, vikizalisha wahitimu wanaotafuta ajira.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie anasema vyuo vya kati ni muhimu kwenye kuzalisha ajira kwa kuwa vyenyewe vinajikita katika kutoa ujuzi badala maarifa pekee.

“Changamoto kubwa ni nchi yetu kuhusudu cheti badala ya ujuzi, jambo ambalo linafanya mtu anayesoma chuo cha kati kuonekana kama kibarua lakini ujuzi wake hauangaliwi kama kitu chenye thamani,”anasema.

Anasema Watanzania wengi wanataka kuwa maofisa kwa kusomea shahada badala ya kuwa watenda kazi na tatizo jingine Serikali inashindwa kupanga mwongozo kamilifu wa njia sahihi katika suala hilo.

Dk Loisulie anasema kutokana na watu wengi kutopenda kufanya kazi ndogo ndogo, baadhi ya vyuo viliamua kubadili na kuwa vyuo vikuu ili kupata hadhi ambayo inapendwa na Watanzania ya kuzalisha maofisa.

Mbunge wa Songwe (CCM), Philipo Mulugo anasema vyuo vya kati vinatengeneza mafundi mchundo ambao wanahitajika kwa wingi katika maeneo mbalimbali viwandani na kwenye miradi.

“Wale wenye shahada na kuendelea mara nyingi sana hawafanyi kazi, kazi yao kubwa ni kusimamia na kutoa maelekezo na kuonyesha. Ni wachache sana wanaweza kufanya kazi kama mafundi mchundo,”amesema Mulugo ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Anasema kada ya kati inasaidia katika kutengeneza ajira kwa vijana nchini kwa kutoa mafundi mchundo.

Anapoulizwa nini athari ya vyuo vya kati kuwa vyuo vikuu, Mulugo ambaye kitaaluma ni mwalimu, anasema vyuo hivyo havijigeuzi kuwa vyuo vikuu bali vimekuwa vikipanda hadhi kwa kuongeza wigo wa ngazi ya elimu wanayoitoa. “Hii inatokana na application (maombi) za wanafunzi kuwa nyingi, kuna njia nyingi za kusoma shahada na sio lazima uende kidato cha tano na sita. Vyuo vilivyokuwa vinatoa diploma bado vinaendelea kuitoa lakini vimeongeza pia shahada,”anasema.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Tunza Malapo amesema kimsingi vyuo vya kati ni vyuo vinavyotumika kuwezesha wanachuo kupata ujuzi mbalimbali kwa ajili ya uzalishaji wataalam kwenye sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, viwanda vikubwa na vidogo.

Anasema kwa msingi huo, anatarajia uwekezaji na uwezeshaji wa vyuo vya kati utaibua vijana wengi wenye ujuzi mbalimbali.

“Hivyo mimi kwa maoni yangu tabia ya kugeuzwa vyuo vya kati kuwa vyuo vikuu siiafiki kabisa, kwani inapunguza uzalishaji wa vijana wengi wenye ujuzi na kuzalisha mameneja wengi ambao hawawezi kufanya kazi za uzalishaji,”anasema.

Anasema kama Serikali inalenga kweli kuwa na uchumi wezeshi wa viwanda, basi vyuo vya kati viwezeshwe kwa kupatiwa wakufunzi na vifaa bora na vya kisasa, ili kuzalisha wahitimu bora wenye ujuzi na uwezo unaoendana na zama zilizopo.

Hata hivyo, Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MENT), Ochola Wayoga anasema baadhi vyuo vya kati vimeanza kuwa ni shida kwa kurudia rudia nguvu kazi wanazozalisha badala kuwa na ubunifu wa maeneo mengi yanayohitaji wataalamu.

“Hatuwezi tukahitaji mafundi seremala tu, magari tu, uashi tu hii dunia ina ujuzi wa ufundi ambao sisi Tanzania hatuna. Kwa mfano, hawafundi watu kutengeneza vijiko ambavyo vinatumika kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo hotelini, migahawani na majumbani,”anasema.

Anasema kuna bidhaa nyingi zinazotumika mara kwa mara ambazo zinaweza kutumika kwenye maeneo mbalimbali badala ya kuagiza kutoka nje.

“Ajira ipi tunayoiongea nafikiri bado tuna mitazamo tofauti, tunaongelea ajira ya kupiga rangi, kusuka,kutengeneza magari lakini ajira ambayo ingeleta ajira ni hiyo ya kuzalisha vitu tunavyoagiza nje ya nchi,”anasema.

Wayoga anasema kwa mtindo huo, vyuo hivyo vitapunguza changamoto ya ajira kwa baadhi kujiajiri lakini kinachotakiwa ni vijana hao kuweza kutengeneza ajira kwa wengine.

“Kwa mfano, mtu amesomea ufundi bomba mimi tangu nifunge bomba sijawahi kumuita mtu anirekebishie lakini kama amejifunza kutengeneza bidhaa mbalimbali anaweza kuuza katika supermarket (maduka makubwa) na hata kusafirisha nje ya nchi,”anasema.

Mzazi, Projest Humphrey anasema vyuo vya kati vinatakiwa kuzalisha watu wenye ubunifu wa kuzalisha bidhaa mbalimbali ambazo zitatatua matatizo ya wananchi.

“Changamoto vyuo vyetu vingi vya kati vinazalisha watoa huduma wengi kuliko wabunifu wanaoweza kubuni teknolojia zinazoendana na mahitaji ya watu nchini,”anasema.

Anataka vyuo vya kati kujielekeza katika kuibua vijana watakaoweza kujikita katika kutengeneza bidhaa zinazotumiwa na watu wengi nchini.

“Huwa najiuliza tunashindwaje kutengeneza vitu vidogo vidogo ambavyo vinatumika karibu kila siku na watu. Hivi vingeweza kutuzalishia ajira kwa watu wetu. Sasa vyuo hivi vijikite katika kuibua vijana wa namna hii,”anasema.

Anasema hilo, litasaidia katika kuvifanya vyuo hivyo kutoa vijana watakaopata ajira wengi kuliko kujikita katika ufundi seremala, ujenzi, ushonaji, upishi ambao sio kila mara mtu anauhitaji.

Related Posts