Dar es Salaam. Kampuni ya huduma za mawasiliano kwa simu za mkononi ya Vodacom Tanzania Plc imewasilisha utetezi katika kesi ya madai ya Dola za Marekani 10 milioni (takribani Sh28 bilioni) zinazodaiwa na mwanahabari Erick Kabendera.
Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, Kabendera anaituhumu kampuni hiyo ya Vodacom kuwa ndio iliyofanikishwa kukamatwa kwake na askari polisi, tukio analoliita kutekwa, na kisha kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi, mwaka 2019.
Kabendera alitiwa mbaroni na askari polisi nyumbani kwake Julai 29, 2019 na kushikiliwa kwa siku kadhaa, kisha akafunguliwa kesi ya uhujumu uchumi.
Katika kesi hiyo Kabendera anadai kuwa kutokana na tukio hilo amepata madhara ya kiuchumi na yasiyo ya kiuchumi, ya kijamii, maumivu ya kiakili na kimaono, hasara ya kutokufurahia maisha hasara ya maendeleo binafsi na hadhi yake katika jamii na kutokuaminiwa kitaaluma.
Hivyo anaitaka kampuni hiyo imlipe kiasi hicho cha fedha kama fidia ya hasara halisi na riba kwa kiwango cha mahakama (asilimia) kuanzia tarehe ya hukumu mpaka kumaliza malipo yote.
Pia, anataka alipwe fidia ya hasara ya jumla kadri mahakama itakavyotathmini, gharama za kesi na nafuu nyingine kadri mahakama itakavyona inafaa
Kesi hiyo ya madai namba 12799/2024 inayosikilizwa na Jaji Mfawidhi Salma Maghimbi imetajwa mahakamani hapo leo Jumanne, Julai 9, 2024.
Kwa mujibu wa hati ya wito wa mahakama kwa wadaawa (pande zote) kufika mahakamani hapo leo, kampuni hiyo ilitakiwa kufika bila kukosa na kuwasilisha nyaraka zake ambazo inatarajia kuzitumia katika utetezi wake.
Hivyo kampuni hiyo imefika mahakamani na kuwasilisha maelezo yake ya utetezi wa maandishi sambamba na pingamizi la awali.
Wakati kesi hiyo ilipoitwa, mbele ya Jaji Maghimbi, Wakili wa Kabendera, Peter Madeleka ameieleza Mahakama kuwa wamepokea nakala ya maelezo ya majibu ya madai ya mteja wake kutoka kwa Wakili wa mdaiwa, Vodacom Gaspar Nyika.
Wakili Madeleka ameieleza kuwa walipokea majibu hayo ya mdaiwa jana na kwamba wanakusudia kuweka pingamizi dhidi ya kesi hiyo.
“Mheshimiwa jaji kuna notisi ya pingamizi, tunaomba kabla ya kuendelea na shauri la msingi tupewe utaratibu wa kusikiliza pingamizi na kwa upande wetu tunaomba lisikilizwe kwa maandishi,” amedai Wakili Madeleka.
Akijibu hoja hiyo Wakili Nyika ameithibitishia Mahakama kuwa kweli wamewasilisha majibu ya utetezi pamoja na pingamizi la awali.
Kuhusu hoja ya Wakili Madeleka kusikiliza pingamizi hilo kwa njia ya maandishi Wakili Nyika amesema kuwa wanakubali pingamizi walilowasilisha lisikilizwe kwa njia ya maandishi.
Katika maelezo hayo ya utetezi ambayo Mwananchi limeiona nakala yake kampuni hiyo inakana tuhuma zote zilizotelekezwa kwake na mwanahabari huyo kuhusu ushiriki wake kufanikisha kukamatwa kwake anakoita kutekwa.
Badala yake, kampuni hiyo imemtaka mwanahabari Kabendera kuthibitisha tuhuma hizo dhidi yake.
Katika pingamizi hilo ililoliibua, kampuni hiyo imetoa hoja ya kisheria dhidi ya usikilizwaji wa kesi hiyo.
Katika pingamizi hilo kampuni hiyo inaiomba Mahakama hiyo iitupilie mbali kesi hiyo bila kuisikiliza ikidai kuwa haina mamlaka ya kuisikiliza kwa madai kuwa imefunguliwa nje ya muda uliowekwa kisheria.
Kutoka na pingamizi hilo, na baada ya kusikiliza hoja za pande zote na kama ilivyo ada mahakama inalazimika kusikiliza na kuamua kwanza pingamizi hilo kabla ya kesi ya msingi.
Hivyo Jaji Maghimbi ameamuru pingamizi hilo lisikilizwe kwa njia ya maandishi, ikielekeza mdaiwa (Vodacom) iwasilishe hoja zake kutetea pingamizi lake hilo Julai 23, 2024 na mdai, Kabendera awasilishe majibu ya hoja za pingamizi hilo Agosti 6, 2024.
Pia Jaji Maghimbi ameelekeza Vodacom kama itakuwa na majibu ya ziada dhidi ya hoja za Kabendera basi iyawasiliashe mahakamani Agosti 13 na akapanga kutoa uamuzi wa pingamizi hilo Agosti 21, 2024.
Ikiwa Mahakama katika uamuzi wake itakubaliana na pingamizi hilo la Vodacom basi itaifutilia mbali kesi hiyo na huo ndio utakuwa mwisho wa kesi hiyo isipokuwa kama Kabendera atakata rufaa Mahakama ya Rufani na ikaamua vinginevyo.
Lakini kama Mahakama itatupilia mbali pingamizi hilo, basi utaendelea na usikilizwaji wa kesi ya msingi na baadaye kuamua kama Kabendera atakuwa amethibitisha madai yake dhidi ya kampuni hiyo au la, kisha itatoa amri kulinga na uamuzi huo utakavyokuwa.
Kwa mujibu wa hati ya madai katika kesi hiyo Kabendera ameeleza matukio yaliyojiri katika simu yake kabla ya tukio la kukamatwa kwake, kuwa ilianza kupoteza mawasiliano na kumfanya ashindwe kupata huduma ya mawasiliano.
Pia Kabendera ameelezea juhudi alizofanya kujua chanzo cha hali hiyo kwa kufanya mawasiliano na mwakilishi wa huduma kwa wateja na hata kutembelea ofisi za kampuni hiyo lakini hakupata ufumbuzi wa tatizo hilo.
Kwa mujibu wa hati hiyo ya madai, hali hiyo ilianza Julai 27, 2019, saa 9:00 alasiri alipoiwasha simu yake ambayo alikuwa ameizima tangu Jana yake usiku na kwamba ndipo alipobaimi kuwa haikuwa na mtandao.
Hivyo aliazima simu nyingine akampigia mtoa huduma kwa mteja kujua mazingira yaliyosababisha kumkatia huduma katika simu yake bila kumjulisha kwanza.
Mwakilishi wa huduma kwa wateja wa Vodacom alimweleza kuwa namba yake ya simu ya Vodacom (+255767456796) ilikuwa na changamoto za kiufundi ambayo ilimhitaji kutoa taarifa katika kituo cha huduma kwa wateja cha karibu kilichopo Tegeta.
Kabendera amemtaka mwakilishi huyo kuelezea tatizo ni nini kabla ya kwenda huko kituoni, lakini mwakilishi huyo alikataa akidai kuwa ni suala nyeti ambalo linamtaka aende binafsi kituoni hapo.
“Hata hivyo (Kabendera alisita kwenda huko kituo cha huduma kwa wateja) kwa kuwa kulikuwa kuna matukio kadhaa ya watu kutekwa ama kutiwa mbaroni walipokuwa wakitembelea kituo cha huduma kwa wateja tangu mwaka 2016.” inasomeka sehemu nyingine ya hati hiyo ya hiyo na kuongeza:
Inaendelea kueleza kuwa Jumatatu, Julai 29, 2019 saa 4:00 asubuhi Kabendera alipiga tena simu ya huduma kwa wateja akimlalamikia kuwa alikuwa akihitaji kutoa fedha kwenye simu yake hiyo kwa ajili ya kumnunulia dawa mama yake aliyekuwa mgonjwa.
Mwakilishi wa Vodacom aliyemhudumia alimweleza kuwa asubiri kidogo ili amuulize meneja wake na alirejea dakika chache baadaye na kumweleza kuwa kesi yake ilikuwa nyeti na kwamba ilikuwa juu ya uwezo wao kuitatua.
Badala yake walimshauri atembelee ofisi zao zilizoko Mliman City asubuhi hiyo.
Hata hivyo, saa 9:00 alasiri siku hiyo hiyo ya Julai 29, ghafla tu simu yake ilianza kufanya kazi, kisha alipoigiwa simu na mwakilishi wa Vodacom ambaye alimtaka (Kabendera) amwelezee tatizo lake na baada ya Kabendera kumuelezea kwa takribani dakika tatu, alikata simu akiahidi kumpigia baadaye kidogo.
Baada ya takribani dakika tatu Kabendera alipokea simu iliyopigwa kutoka huduma kwa wateja Vodacom ambayo aliipokea akabaini kuwa ilikuwa ni sauti ya mwanaume, ambaye alimtaka Kabendera aeleze mahali alikokuwa na kwamba simu hiyo ilikuwa ikihanikiza na kukwaruza kama vile ilikuwa inarekodiwa.
“Kabla ya simu hiyo kukatwa mteja wetu alimsikia huyo aliyempigia simu hiyo akinong’ona kuwa alikuwa nyumbani kwake na kuongeza kuwa sogea karibu na nyumba yake,” inasomeka sehemu nyingine ya hati hiyo ya madai.
Kwa mujibu wa hati hiyo, maelezo hayo yalimshtua Kabendera, na akakimbia sehemu ya juu ya nyumba yake ambako aliweza kuona magari kadhaa ambayo hakuyafahamu, karibu ya nyumba yake.
Kisha lilitokea gari lingine aina ya Toyota Alphard lililoegeshwa mbele ya magari hayo upande wa kulia mwa nyumba yake, halafu wakashuka watu wanne ambao walijitambulisha kuwa maofisa wa polisi lakini walikataa kutoa utambulisho. Walimfunga pingu kumshikilia kizuizini kwa siku mbili.
Hati hiyo inaendelea kueleza kuwa wakati wa mahojiano, maofisa wa polisi walifika katika chumba cha mahojiano wakiwa na karatasi zilizochapishwa kutoka katika kompyuta (printout) za akaunti pesa ya simu na za namba simu alizokuwa amezipiga kwa mwaka mzima.
Hivyo walimhoji lengo la kila muamala alioufanya kwa mwaka mzima nyuma yake na pia walimhoji uhusiano wake na watu aliokuwa amewasiliana nao miaka kadhaa.
Kabendera analalamika kuwa polisi na Serikali walitoa taarifa kadhaa zenye mgogoro kwa umma kuhusiana na ‘kutekwa’ kwake na kwamba walimtuhumu kwa kutokuwa raia na kumkashfu Rais (wa wakati huo) John Magufuli.
“Hatimaye alishtakiwa mahakamani kwa makosa ya utakatishaji fedha, uhujumu uchumi na ukwepaji kodi na matokeo yake walimuweka chini ya ulinzi mkali katika mahabusu ya Gereza la Segerea.
“Na usikilizwaji wa kesi yake mahakamani uliahirishwa mara 12 upande wa mashtaka ukiomba muda zaidi wa upelelezi,” inaeleza hati hiyo.
Inaeleza zaidi kuwa wakati akiwa mahabusu mama yake, Verdiana Mujwahuzi alifariki dunia na hakuruhusiwa kuhudhuria mazishi yake na kwamba hata yeye mwenyewe alikuwa na tatizo la kiafya.
Pia, inaeleza kuwa kutokana na hali hiyo inaeleza kuwa aliamua kukiri makosa na kulipa fidia ya Sh273 milioni ili atoke mahabusu na kwamba baada ya kuachiliwa marafiki na familia yake walimweleza kuwa walipigiwa simu na polisi wakiwaonya kutokumtembelea mahabusu na kwamba vinginevyo wangepata hatari.