Watanzania waaswa kuunga mkono juhudi za REA

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Watanzania wameaswa kuendelea kuunga mkono juhudi za Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuchangamkia fursa mbalimbali za nishati zinazotolewa, ikiwemo fursa ya mkopo nafuu wa uwezeshaji wa ujenzi na uendeshaji wa vituo vidogo vya mafuta (petroli na dizeli) vijijini.

Hayo yamebainishwa, Julai 8, 2024, na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi na Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu, alipokuwa akitembelea banda la REA kwenye maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa. Alisema kuwa sekta ya nishati ni kichocheo cha ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi duniani kote.

Ameeleza kuwa sekta hizo ni pamoja na viwanda vidogo, vya kati, na vikubwa, ambavyo uzalishaji wa malighafi unategemea upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu, na inayopatikana kwa wakati wote.

“Natoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kuchangamkia fursa kama mikopo ya ujenzi na uendelezaji wa vituo vidogo vya mafuta vijijini, pamoja na fursa nyingine ikiwemo upatikanaji wa umeme vijijini, hasa katika maeneo ambayo hayajajiunga na huduma ya umeme licha ya kuwa umeme umefika,” alisema Balozi Kingu.

“Natumia nafasi hii kuipongeza Menejimenti ya REA kwa kuendelea kutekeleza maelekezo ya Bodi ipasavyo. Kazi yetu kubwa ni kuhakikisha maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu sekta ya nishati vijijini tunayatekeleza na kuyasimamia ipasavyo,” aliongeza.

Akizungumzia kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, Balozi Kingu alisema REA imeanza kutekeleza kwa vitendo matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

“Tumesaini makubaliano ya kushirikiana na Jeshi la Magereza. Tumeanza na taasisi hii kwa sababu inatumia mkaa na kuni kwa kiasi kikubwa kama chanzo cha nishati, na kwa kuwa inahudumia zaidi ya watu 100. Ndani ya kipindi cha miaka miwili, tarajieni mabadiliko makubwa kwenye matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia,” alieleza.

Related Posts