Raia wa Irani walimchagua Jumamosi, Masoud Pezeshkian, mgombea mwenye msimamo wa wastani kuwa rais wao ajaye katika kura ya marudio iliyomshindanisha na Saeed Jalili, mhafidhina mwenye msimamo mkali na msuluhishi wa zamani wa nyuklia anaepinga vikali mataifa ya Magharibi.
Pezeshkian, daktari wa upasuaji wa moyo,amekuwa mbunge wa Bunge la Iran tangu 2008. Alihudumu kama waziri wa afya wa nchi hiyo kuanzia mwaka 2001 hadi 2005 chini ya rais wa wakati huo Mohammad Khatami, ambaye alionekana kama mwanamageuzi.
Rais huyo mteule mwenye umri wa miaka 69 ameapa kujenga uaminifu kati ya “inayoweza kuwa serikali ya mrengo wa wastani” na raia. Kampeni yake ililenga kuwarejesha wafuasi waliovunjwa moyo wa kambi ya wanamageuzi.
Muungano mkuu wa wanamageuzi wa Iran ulimuunga mkono Pezeshkian, kwa kuidhinishwa na marais wa zamani Khatami na Hassan Rouhani.
Nani mwenye nguvu zaidi nchini Iran?
Wakati wa kampeni, Pezeshkian hakuahidi mabadiliko yoyote makubwa kwa utawala wa Iran unaofuata misingi ya Uislamu wa madhehebu ya Kishia, unaodhibitiwa na viongozi wa kidini.
Pezeshkian ameahidi hadharani utiifu wake kwa Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo Ayatollah Ali Khamenei na hana nia ya kukabiliana na watendaji wakuu wa idara za usalama za jamhuri na watawala wa kidini.
Katika mfumo wa kisiasa wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu, rais si mkuu wa nchi bali ni mkuu wa serikali, anayechaguliwa kwa kura za wananchi.
Mamlaka makubwa zaidi yako kwa kiongozi mkuu wa nchi, nafasi ambayo Khamenei ameshikilia tangu 1989.
Soma pia:Rais mteule wa Iran kuapishwa rasmi mwezi Ujao
Rais, kwa mfano, hawezi kufanya mabadiliko yoyote kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, wala sera ya kigeni au ya usalama. Kauli ya mwisho juu ya mada zote hizo ni ya Khamenei.
Zaidi ya hayo, karibu kila mhimili wa serikali ya Irani bado unadhibitiwa kwa kiasi kikubwa na watu wenye msimamo mkali, na kuwekea kikomo mamlaka ya rais juu ya utawala wa nchi.
“Sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu, kama ilivyoelezwa na Ali Khamenei, kiongozi mkuu wa Iran, haziingii ndani ya maamuzi ya rais,” alisema Ighan Shahidi, mtafiti wa Iran katika Chuo Kikuu cha Cambridge.
“Sera hizi zinahusu maamuzi ya kiongozi mkuu na taasisi za juu za usalama, ambazo zina mipango ya muda mrefu ya kupanua ushawishi wa kikanda wa Iran, kama chombo muhimu cha kuongeza uwezo wake wa mazungumzo na athari kwa mienendo ya kikanda,” aliiambia DW.
Iran yakabiliwa na changamoto lukuki za kiuchumi
Ingawa haijulikani wazi iwapo Pezeshkian ataweza kutekeleza hata mabadiliko ya kawaida, kama afisa mkuu aliyechaguliwa nchini humo, rais anaweza kushawishi mwelekeo wa sera ya Iran.
Pia atahusika moja kwa moja katika kuchagua mrithi wa Khamenei anayezeeka, ambaye sasa ana umri wa miaka 85.
Uchaguzi wa rais wa Iran ulifanyika katikati mwa mvutano mkubwa wa kikanda kuhusu vita kati ya Israel na washirika wa Iran Hamas huko Gaza na Hezbollah nchini Lebanon.
Ongezeko lolote katika mzozo huo linaweza kuiingiza Iran katika mzozo wa moja kwa moja na Israeli. Pia kuna hisia kubwa za kutoridhika kwa raia kuhusiana na hali mbaya ya uchumi wa Iran.
Nchi hiyo inakabiliwa na ukosefu mkubwa wa ajira, wakati mfumuko wa bei umekuwa ukipanda karibu asilimia 40, na thamani ya sarafu ya Iran, rial imeshuka pakubwa.
Theluthi moja ya raia milioni 90 wa nchi hiyo sasa wanaishi katika umaskini, kulingana na data rasmi, ikiashiria ongezeko la watu milioni 11 katika kipindi cha miaka 13 iliyopita.
Soma pia:Mataifa ya Ghuba yatuma salamu kwa raisi mpya wa Iran
Hamid Babaei, profesa msaidizi katika Shule ya Usimamizi ya IESEG mjini Paris, aliiambia DW kuwa changamoto kubwa za Pezeshkian zitakuwa kukuza ukuaji wa uchumi na kudhibiti mfumuko wa bei.
“Katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, ongezeko la ukuaji wa uchumi limekuwa karibu sufuri. Mfumuko wa bei nchini Iran ni suala la muda mrefu, ambalo linasababishwa na ufinyu wa bajeti na utanuzi wa matumizi ya fedha,” alisema.
Babaei anaamini kuwa “hakuna uwezekano mkubwa” kwamba Pezeshkian ataweza kushughulikia changamoto hizo za kiuchumi.
“Inaweza kusemwa kuwa viashiria vya uchumi mkubwa wa Iran viko mwanzoni mwa hali ya kushuka, ambayo inaonekana haiwezekani kwa rais yeyote kudhibiti,” alisisitiza.
Je, Pezeshkian anaweza kushirikiana na Magharibi?
Bado, kwenye kampeni, Pezeshkian aliahidi “kurekebisha” uchumi. Sehemu ya mpango wake wa kufanya hivyo ilikuwa ahadi yake ya kuzifikia nchi za Magharibi kujaribu “kuiondoa Iran katika kutengwa kwake” na kuikomboa nchi hiyo kutokana na vikwazo vya kimataifa.
Rais huyo mpya pia anapendelea kufufuliwa kwa makubaliano ya nyuklia ya 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani.
Mkataba huo umekuwa wa kusuasua tangu Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump alipoiondoa Washington katika mapatano hayo mwaka 2018 na kuiwekea tena vikwazo Tehran.
Anaweza kutuliza kutoridhika kuhusu sera kali za kijamii?
Zaidi ya hayo, Pezeshkian amezungumza dhidi ya sera kali ya hijabu ya taifa hilo la Kiislamu, akiahidi kupinga “kikamilifu” doria za polisi kuitekeleza.
Kufunika nywele za mtu kwa hijabu, au hijab, ni lazima kwa wanawake nchini Iran. Ukiukaji wa sheria hiyo unaadhibiwa vikali na mamlaka za kidini za nchi.
Soma pia:Pezeshkian ashinda duru ya pili ya uchaguzi wa rais Iran
Mnamo Septemba 2022, kifo cha Jina Mahsa Amini mwenye umri wa miaka 22 chini ya ulinzi wa polisi kilisababisha maandamano makubwa ya kuipinga serikali. Mwanamke huyo kijana alikuwa amekamatwa na wale waliojiita polisi wa maadili katika taifa hilo, ambao walidai kuwa alishindwa kufunika nywele zake vizuri.
Ukandamizaji wa kikatili uliofanywa na mamlaka dhidi ya waandamanaji uliacha nyufa kubwa ndani ya jamii ya wa Iran.
Hakuna maboresho yanatarajiwa?
Ighan Shahidi aliiambia DW kuwa hatarajii maendeleo yoyote nchini Iran katika masuala ya haki za binadamu, hasa kwa wanawake na wanaonyanyaswa kidini kama vile jamii ya Bahai, hata chini ya urais wa Pezeshkian.
“Kilicho wazi ni kwamba, kuna maagizo na kanuni zilizotolewa na mashirika na taasisi nyingine za ngazi ya juu za serikali ya Iran, kama vile Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni, ambazo zimepelekea kukiukwa haki za wananchi wa Iran.” Alisema.
“Rais haonekani kuwa na mamlaka au uwezo wa kufanikisha mabadiliko yoyote au maboresho katika visa kama hivyo.”