Aziz KI amaliza utata Yanga, Baleke vipimo freshi

WAKATI Jean Baleke akianza rasmi tizi na Yanga leo, kiungo mshambuliaji wa klabu hiyo, Stephane Aziz KI amemaliza utata juu ya hatma ya kusalia katika timu hiyo au kuondoka baada ya kutua alfajiri ya kuamkia leo kisha saa 8 mchana amezungumza na Wanayanga ‘laivu’ kusisitiza bado yupo sana Jangwani.

Aziz aliyezua sintofahamu baada ya kudaiwa kutosaini mkataba mpya na baadhi kuvumisha huenda akaondoka klabuni hapo akihusishwa na ofa za Azam, Simba na klabu za Afrika Kusini, amemaliza utata kwanza kwa kutua alfajiri na kutolewa kininja kwenye Uwanja wa Ndege.

Aziz KI, amewasili alfajiri ya leo kwa Ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia lakini akatoka kimkakati lwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal 3.

Alichofanya Azizi Ki, kwanza akamtanguliza mbele mfanyakazi mmoja wa uwanja huo  wa ndege akiwa mabegi makubwa sita aliyotua nayo, kisha ikawa ni zamu ya ofisa mmoja wa Yanga, Godlisten Anderson ‘Chicharito’ aliyekuja kumpokea hapo kumpenyezea kofia maarufu kwa jina la kepu, ambayo kiungo huyo ilipomfikia akatoka akiwa ameishusha kijanja mithili ya mtu asiyetaka kujulikana kama amefika.

Hatua ya tatu akatoka akiwa peke yake huku Chicharito akitangulia mbele wakiachana kwa hatua sita na kiungo huyo kisha kupakiwa kwenye gari moja aina ya Toyota Alphard iliyotoka uwanjani hapo kwa kasi.

Hatua ya nne mara baada ya kufika nje ya uwanja wa ndege kiungo huyo akakuta gari nyingine aina ya Toyota Harrier ikimsubiri kisha kupandishwa humo, huku Ile Alphard ikiondoka na mabegi yake pekee.

Ujio wa Azizi Ki ambaye ndiye Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita akimaliza na mabao 21 umewashusha presha mashabiki wa Yanga ambao walidhani angeweza kuondoka na leo mchana amezungumza na Wanayanga na kuweka bayana kwamba bado yupo sana klabuni hapo.

Akizungumza kupitia Yanga App, Aziz KI amesema yeye bado yupo sana kwani amesaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kuitumikia timu hiyo na zile taarifa kwamba anaondoka zilikuwa ni blah blah tu, kwani bado ana kazi kubwa ya kufika mbali na timu hiyo hasa kimataifa.

“Bado nipo sana Yanga, kwani kuna projekti kubwa na klabu hiyo na hasa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” amesema Aziz KI aliyeifungia Yanga jumla ya mabao 30 katika misimu miwili ya Ligi Kuu, mbali na kushirikiana na wenzake kuifikisha timu fainali ya Kombe la Shirikisho na robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika sambamba na kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu, matatu ya Kombe la Shirikisho na mawili ya Ngao ya Jamii.

Hayo ya Aziz KI yakiwa hivyo, straika wa zamani wa Simba, Jean Baleke aliyesaini mkataba wa mwaka mmoja Yanga, amefuzu vipimo vya afya juzi na tayari ameanza mazoezi na wenzake kambini.

Ujio wa Baleke ni habari mbaya kwa Joseph Guede, ambaye rasmi amelazimika kuhamishiwa Singida Black Stars kumpisha Mkongomani huyo.

Guede alimaliza mkataba wa miezi sita ya awali na mabosi wa timu hiyo na kuamua kutokumuongezea mkataba mpya.

Mkongomani huyo, alianza mazoezi ya gym yaliyofanyika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es salaam, akiwa na wachezaji wenzake wa timu hiyo yake mpya.

Baleke anaifanya Yanga kuwa na mastaa wapya sita kambini kwao akitanguliwa na kipa Abubakar Khomeny, beki Chadrack Boka, viungo Clatous Chama aliyekuwa Simba, Aziz Andambwile na mshambuliaji Prince Dube kutoka Azam FC.

Kikosi cha Yanga, kesho jioni kinatarajiwa kuhama kutoka gym kwenda kujifua kwenye Fukwe za Coco (Coco Beach) kuendeleza hesabu zao za kujiweka sawa kabla ya kuanza msimu mpya wa mashindano.

Taarifa zinasema, mazoezi hayo ufukweni yataongozwa na kocha mkuu wa timu Miguel Gamondi, ambaye tayari ameshawasili nchini na kuungana na wachezaji wake pamoja na wasaidizi wake ambao walishatangulia kambini.

Related Posts