Aziz Ki atua Dar kutegua kitendawili

Dar es Salaam. Taarifa itakayowashusha presha mashabiki wa Yanga ni kwamba hatimaye kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Stephanie Aziz KI, amewasili nchini huku akitolewa Uwanja wa Ndege kininja.

Aziz KI, amewasili nchini alfajiri ya leo Julai 10, 2024 akitokea mapumziko nchini kwao kwa Ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia lakini akatoka kimkakati uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere terminal 3.

Alichofanya Azizi Ki, kwanza akamtanguliza mfanyakazi mmoja wa Uwanja wa Ndege kutangulia mbele  na mabegi yake makubwa sita aliyotua nayo.

Hatua ya pili ikawa Ofisa mmoja wa Yanga Godlisten Anderson ‘Chicharito’ aliyekuja kumpokea uwanjani hapo kumpenyezea kofia maarufu kwa jina la kepu, ambayo kiungo huyo ilipomfikia akatoka akiwa ameishusha kijanja mithili ya mtu asiyetaka kujulikana.

Hatua ya tatu akatoka akiwa peke yake huku Ofisa huyo wa Yanga akitangulia mbele wakiachana kwa hatua sita na kiungo huyo kisha kupanda kwenye gari moja aina ya Toyota Alphard iliyotoka uwanjani hapo kwa kasi.

Hatua ya nne mara baada ya kufika nje ya uwanja wa Ndege kiungo huyo akakuta gari nyingine aina ya Toyota Harrier ikimsubiri kisha kupanda humo huku ile Alphard ikiondoka na mabegi yake pekee.

Ujio wa Azizi Ki ambaye ndiye mfungaji Bora wa Ligi msimu uliopita akimaliza na mabao 21 utawashusha presha mashabiki wa Yanga ambao wanadhani anaweza kuondoka.

Yanga bado haijatangaza kwamba Azizi Ki ameongeza mkataba lakini Mwananchi linafahamu kwamba kiungo huyo raia wa Burkina Faso bado ataendelea kuitumikia timu hiyo kufuatia kukubaliana na mabosi wa timu hiyo kwamba atasalia.

Pia, kupitia mitandao ya kijamii ya Yanga imetangaza kuwa staa huyo atazungumza mchana wa leo.

Related Posts