Balozi Mette aaga rasmi, Makamba azungumzia mchango wake

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amemuaga Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette Norgaard Dissing Spandet baada ya kumaliza muda wake wa kuhudumu hapa nchini.

Waziri Makamba amempongeza Balozi Mette jana Jumanne Julai 9 2024 jijini Dar es Salaam katika ofisi ndogo za wizara hiyo, kwa kazi nzuri aliyoifanya nchini, sio tu kwa kukuza na kudumisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Denmark, bali kwa mchango wake kwenye utekelezaji wa programu na miradi ya kiuchumi na kijamii iliyochangia ukuaji wa maendeleo.

Aidha, Waziri Makamba amempongeza Balozi Mette kwa mchango wake alioutoa katika kutafuta suluhu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia ikiwamo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na masuala ya amani na usalama. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba (kulia) akimsikiliza Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette Norgaard Dissing Spandet.

Kwa upande wake, Balozi Mette amesema licha kuendelea kukua kwa uhusiano wa kidiplomasia bado juhudi zaidi zinahitajika kukuza kiwango cha biashara na uwekezaji Tanzania na Denmark.

Balozi Mette ameishukuru Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa  Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano mzuri alioupata wakati wote akitimza majukumu yake hapa nchini.

“Natambua kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, licha kumaliza kipindi changu cha kuhudumu kama balozi, nitaendelea kutoa mchango wangu kwa namna mbalimbali ili kuhakikisha kiwango cha biashara na uwekezaji baina ya Tanzania na Denmark kinaongezeka,” amesema Balozi Mette.

Tanzania na Denmark zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali zikiwamo za kilimo, afya, elimu na biashara na uwekezaji.

Related Posts