Dili jipya la Lawi hadharani

Wakati Simba ikiondoka nchini juzi kwenda Misri kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao bila Lameck Lawi, taarifa ikufike nyota huyo wa Coastal Union yupo zake bize akipambana kukamilisha safari yake ya kwenda Ubelgiji.

Beki huyo juzi alionwa na Mwanaspoti akiingia na kutoka katika ubalozi wa Ubelgiji na alithibitisha kuwa ana mipango ya kwenda nchini humo.

Wakati Lawi akionekana ubalozini hapo, taarifa kutoka ndani ya Coastal Union umefichua beki huyo atauzwa nchini humo kwa moja ya klabu za huko.

Bosi mmoja ndani ya Coastal Union aliongeza Lawi akiuzwa Ubelgiji klabu yao itavuna fedha nyingi zaidi kushinda zile za Simba, Sh206 milioni ilizotaka kuzitumia kumnunua beki huyo.

“Coastal Union tayari tulishawarudishia fedha zao hao Simba, kama wanasema watafungua hiyo kesi shauri yao sisi tutamuuza beki wetu Ulaya, tutapata fedha nyingi zaidi,” alisema bosi huyo.

“Hapa kinachosubiriwa ni taratibu za safari yake kukamilika ili aondoke, tumeliangalia hili kwa upana mkubwa kwanza kwetu Coastal litatupa fedha nyingi, tutaisaidia Tanzania kama kijana kama huyu atakwenda huko lakini hata mchezaji atakwenda kunufaika zaidi.”

Simba ilitoa taarifa ya kukamilisha usajili wa beki huyo wa timu ya Taifa, Taifa Stars na kumtangaza kwenye mitandao ya kijamii, kabla ya viongozi wa Coastal kukanusha haijamuuza.

Beki huyo hatembei peke yake hapa Dar es Salaam inadaiwa Coastal imempa mtu maalumu anayekwenda naye maeneo mbalimbali.

“Hao watu wa hizo klabu zenu (kubwa) hawaeleweki. Si mnamuona yuko na mtu. Yule ni mtu maalumu ambaye hatakiwi kuachana na Lawi hata kwa sekunde moja,” alisema bosi mmoja wa Wagosi.

Related Posts