Hakimu akwamisha kesi ya uvujishaji mitihani

Dar es Salaam. Kesi ya  kuvujisha Mtihani wa Taifa wa darasa la saba mwaka 2022 inayowakabili mshtakiwa, Patrick Chawawa na wenzake  imeshindwa kuendelea na usikilizwaji  baada ya Hakimu Mkazi Mkuu, Amir Msumi anayendesha shauri hilo kupata uhamisho kwenda Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Wakili wa Serikali, Judith Kihampa ameieleza Mahakama hiyo kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kusikilizwa kesi ndogo ya msingi kutokana na hakimu anayeendesha shauri hilo kuhamishwa na hawajaleta shahidi.

“Shahidi hatujaleta kutokana na hakimu kupata uhamiasho hivyo tunaiomba Mahakama hii ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,”amesema Kihampa.

Baada ya maelezo hayo, Msumi amesema kuwa yeye amehamishiwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha hivyo amewataka washtakiwa hao wasubiri Ili waweze kupangiwa hakimu mwingine.

“Nimehamishwa  Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, mimi sitaendelea na shauri hili hivyo msubiri  kupangiwa hakimu mwingine,” amesema Msumi. 

Kesi hiyo imeahiriahwa hadi Julai 23, 2024 kwa ajili ya kutajwa huku washtakiwa wakiwa nje kwa dhamana.

Mbali na Chawawa washtakiwa wengine  ni Jahnson Ondieka , Theresia Chitanda, Elinami Sarakikya, Joyce Nyanyakila na Gladius Roman, Dorcas Muro, Alcheraus Malinzi,Jacob Adagi na Joel Ngome.

Inadaiwa kati ya Oktoba 2, 2022 na Oktoba 12, 2022 sehemu isiyojulikana mshtakiwa Malinzi  akiwa na nia ya kudanganya alitengeneza nyaraka za uongo za mtihani wa somo la uraia darasa la saba akijifanya ni halali na umeandaliwa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).

Pia, tarehe hiyo na sehemu isiyojulikana mshtakiwa Malinzi akiwa na nia ya kudanganya alitengeneza nyaraka za uongo za mitihani wa somo la maarifa ya jamii darasa la saba akidai umeandaliwa na Necta.

Katika shtaka lingine mshtakiwa Adagi na Ngome wanakabiliwa na shtaka moja la kuvujisha mitihani ya Taifa ya darasa la saba, kinyume cha sheria.

Related Posts