MASHABIKI wa Yanga wamepata presha ya ghafla wakati wenzao wa Simba wanacheka, huku wakiomba dua mbaya kiungo Stephanie Aziz KI aondoke Jangwani, lakini kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi ameibuka akisema “nimkute Avic haraka”.
Hilo limekuja baada ya Rais wa Yanga, injinia Hersi Said akiwa nchini Afrika Kusini kuviambia vyombo vya habari hatma ya Aziz KI bado haieleweki na hajasaini mkataba mpya na timu hiyo.
Hersi akaenda mbali zaidi akiongeza kuna uwezekano wa asilimia 60 kwa Aziz KI kusalia, pia zipo asilimia 40 za mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akimaliza na mabao 21 kuondoka.
Akizungumza na Mwanaspoti wakati akiwa njiani kurejea kazini, Gamondi alisema hana taarifa za Aziz KI kuondoka na anachotaka ni kumkuta kambini kwao Avic Town, Kigamboni, Dar es Salaam.
Gamondi alisema bado Aziz KI yupo kwenye hesabu zake kubwa kwa msimu ujao na mabosi wake hawajamweleza lolote juu ya kuondoka kwa kiungo huyo.
“Sijasikia wala sijaambiwa. Kuna mawasiliano yangu na viongozi kuhusu hilo hawajaniambia kama ataondoka. Ninachojua au ninachohitaji ni kukutana naye kwenye maandalizi ya msimu mpya,” alisema Gamondi ambaye mabosi wa Yanga wanamjua kwa msimamo wake mkali kwa kile anachotaka.
“Moja ya sifa kubwa ya timu kubwa ni wakati kama huu kutobomoa timu yake bora na kuwabakisha wachezaji wako bora ambao bado unawahitaji, hilo nawaachia wao.”
Wakati Gamondi akiyasema hayo taarifa kutoka ndani ya Yanga zinasema ndani ya saa 72 zijazo kiungo huyo atakuwa ametua nchini kumaliza utata juu ya hatima yake.
Tayari Meneja wa Aziz KI, Zambro Traore yupo nchini kwa takribani siku tano huku Hersi alikuwa akitarajiwa kurejea nchini jana akitokea Afrika Kusini.
Aziz KI anatajwa kuwaniwa na klabu mbalimbali za Afrika Kusini na Afrika Kaskazini, zikipishana kuwania saini yake zikivutiwa na miaka miwili aliyokuwa Yanga
Wakati huohuo, Yanga imeanza maandalizi yake kwa ajili ya msimu mpya kambi yao ikianza na mastaa watatu wapya ambao wawili kati ya hao ndio walioanza mazoezi kisha wakafunguka kauli za kibabe mapemaa.
Kwenye mazoezi ya Yanga yaliyoanzia gym juzi, iliwapokea kipa Abubakar Khomeiny na mshambuliaji Prince Dube huku beki Chadrack Boka akikosa mazoezi hayo ya kwanza.
Wakati Dube akianza mazoezi na timu yake hiyo, ameliambia Mwanaspoti, kama kuna kitu anakisubiri ni kuanza kuichezea timu hiyo akizungukwa na viungo bora.
Dube alisema kiu yake kubwa ndani ya Yanga ni kuhakikisha anapata mataji lakini ana kiu kubwa ya kuisaidia timu hiyo kufunga mabao mengi akitumia ufundi wa viungo bora anaokutana kwa mabingwa hao.
“Kitu nasubiri ni kuanza kucheza, nina hamu ya kucheza sana, kwa sasa nataka kujijenga kuwa imara kwa mazoezi haya magumu yatakayotusaidia,” alisema Dube.
“Mimi ni mshambuliaji kama kuna kitu ambacho kinanifanya kutamani kuanza kucheza hapa Yanga ni kuungana na timu yenye viungo bora kama hii,kila mshambuliaji angependa kucheza eneo kama hili.
“Unakuwa na uhakika wa kupata pasi nzuri zitakazotusaidia kufunga, ukiacha viungo hata mabeki wa pembeni hapa wana ubora mkubwa wa kutengeneza krosi nyingi.
Wakati Dube akiyasema hayo, Boka alisema hajaja Yanga kujaribu ila kuendeleza makali yake na kwa namna kikosi kilivyo na moto basi anaweza kuwa zaidi.
Alieleza kwamba amekutana na viongozi wa klabu hiyo na wamemuelezea malengo ya timu lakini anachoahidi ni kuifanyia kazi kubwa ndani ya kikosi hicho.
“Ukienda Congo Yanga ndio timu inayojulikana zaidi kutokana na Wakongomani wengi waliopita hapa walivyofanikiwa kwa hiyo, haikuwa kazi ngumu kwangu kusimamia maamuzi baada ya Simba kumfuata.
“Sijaja kukaa benchi ila kucheza maana naamini kwenye malengo na ubora niliokuwa nao ijapokuwa nafahamu kuwa kikosi hiki kina wachezaji wenye uwezo mkubwa.
Boka amesema alipokuwa anakuja mjini alikutana na Max Nzengeli uwanja wa ndege na hapo ndipo walipoanza kuzungumzia ligi ya Tanzania ilivyo na ushindani wake kwa jumla.
“Max aliniambia ushindani wa ligi ulivyo bila kusahau upande wa kikosi cha Yanga na alinisisitiza sana kupambana kwa nguvu zote ili kuweza kupata nafasi zaidi kwa wachezaji wote ni bora ndio maana wamesajiliwa timu kubwa kama Yanga.”