JIWE LA SIKU: Ujio wa Chama unavyotishia ufalme wa Mudathir Yanga

NI wazi kusajiliwa kwa kiungo mshambuliaji, Clatous Chama kutoka Simba kwenda Yanga, ni jambo la furaha kwa viongozi na mashabiki wa Yanga kwa ujumla na pigo kwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi, ambao wapo waliotaka aondoke, lakini sio kumwona akienda Jangwani.

Chama anatisha. Takwimu zake uwanjani zinatisha. Ni mchezaji ambaye anaweza kubadili upepo wa mechi wakati wowote ndio maana hamna shabiki wa Simba aliyetamani kumuona akienda Yanga, hata wale ambao walikuwa wakisema wamemchoka. Kama kuondoka walitaka kumuona akitoka nje kabisa ya mipaka ya nchi hii na sio kuhama kutoka mtaa mmoja wa Kariakoo hadi mwingine.

Wakati mashabiki wa Jangwani wakitamba kumpata Mwamba wa Lusaka, jambo lililo wazi ni kuna mtihani mkali kwa kocha Miguel Gamondi. Huu ni mtihani ambao wakati mwingine huitwa mtihani mzuri, pale unapokuwa na machaguo mengi ya kufanya.

Kwa jicho la haraka haraka, unaweza kusema kutua kwa Chama kunamweka Mudathir Yahya katika hatari zaidi ya kupoteza namba sambamba na baadhi ya wachezaji wengine ambao msimu uliopita walikuwa wakipata nafasi mara kwa mara.

Unaweza kujiuliza kwanini Chama ilihali Yanga imetambulisha takribani wachezaji watano akiwemo beki, Chadrack Boka, kiungo Aziz Andambwile na washambuliaji Prince Dube na Jean Baleke.

Kwanza eneo analocheza Chama wapo Aziz KI, Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli ambao msimu uliopita ni moja kati ya pacha bora na wamekuwa na msimu mzuri wakicheza pamoja.

Ubora alioonyesha Chama tangu atue Msimbazi mwaka 2018 akicheza kwa takribani misimu sita sasa umeifanya Yanga kutamani saini yake na hatimaye msimu huu ikafanikiwa.

Ni wazi kwa kiwango chake hakuna kocha anayeweza kumkataa na kumuweka benchi kiungo huyo mwenye uwezo wa kupiga pasi zinazoweza kuamua mechi.

Msimu uliopita kama kawaida eneo la langoni alidumu Djigui Diarra, eneo la beki kuna Dickson Job na Ibrahim Abdullah ‘Bacca’, Yao Kouassi na Nickson Kibabage, viungo wa ulinzi, Khalid Aucho na Mudathir Yahya, viungo washambuliaji, Aziz KI, Pacome na Nzengeli huku washambuliaji Clement Mzize.

Msimu huu, Mudathir hakuwa akicheza sana eneo la kiungo mkabaji baada ya kocha wa Yanga, Miguel Gamondi kumbadilisha na kumchezesha kama winga.

Kama Chama ataingia kwenye mfumo wa Gamondi basi kuna mchezaji mmoja atatoka ili kumpisha kiungo huyo na kutimiza ile idadi ya wachezaji 11.

Kwa jicho la haraka unaweza kusema Nzengeli aanzie benchi kumpisha Chama, lakini kiufundi ndio mchezaji aliyempa vitu vingi Gamondi.

Msimu uliopita Nzengeli, ndiye mchezaji aliyecheza karibu kila mechi akizunguka uwanja mzima yaani akiisaidia timu kukaba, kushambulia na hata kufunga mabao ambayo yamekuwa na msaada kwa Yanga, ndio maana haikuwa ajabu kumaliza na mabao 11 na asisti mbili katika Ligi Kuu mbali na mabao na asisti katika michuano ya Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hivyo hadi sasa Nzengeli ana nafasi ya kubaki kikosini kubwa zaidi ya Mudathir, ambaye nusu msimu alihudumu nafasi ya winga lakini si kila mechi alianza, wakati mwingine alianzia benchini.

Unaweza sema sasa Mudathir ndiye atakayempisha Chama kutokana na nafasi aliyokuwa anacheza na muda alioupata akitokea benchini na kuisaidia Yanga kubadilisha matokeo dakika za jiooni.

Hata hivyo, uamuzi kamili wa nani aanze katika kikosi kipya cha Yanga upo mikononi mwa kocha Gamondi ambaye msimu wa kwanza akiwa Jangwani ameiwezeha timu kutetea kwa mara ya tatu mfululizo ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho na kuipeleka timu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupita miaka 25.

Utamu zaidi ikafika robo fainali na kama sio kudhulumiwa bao la Stephane Aziz KI mbele ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, huenda mambo yangekuwa mengine, kwani matokeo ya jumla ya mechi baina yao yaliamuriwa kwa penalti na Mamelodi kwenda nusu fainali na kukwamishwa na Esperance wa Tunisia.

Related Posts