Moshi. Neema Mmasy, mchumba wa muuguzi katika Hospitali ya Rufaa KCMC, Lenga Masunga (38), aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha ameeleza walichozungumza mara ya mwisho, alipomtaarifu ametoka kazini.
Amesema walikuwa na utaratibu wa kuwasiliana mara kwa mara, wakati wa kwenda na kutoka kazini.
Akizungumza na Mwananchi amesema Julai 2, 2024 saa 10.00 jioni waliwasiliana, akamtaka aendelee na majukumu yake akieleza wangewasiliana baadaye.
Amesema ilipofika saa tatu usiku alishangaa kuona amekuwa kimya hajamtafuta, ndipo alipompigia simu lakini haikupatikana na hata alipomtumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS) haukujibiwa.
Muuguzi huyo katika idara ya masikio, pua na koo anadaiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha Julai 2, 2024 nyumbani kwake katika Mtaa wa Rau Pangaleni, wilayani Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na KCMC, Masunga alikuwa mapumziko ya siku mbili Julai 2 na 3, akitakiwa kuwapo kazini Julai 4, lakini hakuonekana hali iliyoibua wasiwasi na kusababisha uongozi wa hospitali kumtafuta kupitia simu zake za mkononi ambazo hazikupatikana mpaka sasa.
“Nilipoona hajanitafuta nikachukua jukumu la kumtafuta, nilimpigia simu zake hazikupatikana, nikamtumia meseji ili nilale haikujibiwa, ikabidi nilale maana niliwaza huenda simu yake imezima chaji,” amesema Neema katika mahojiano na Mwananchi leo Jumatano Julai 10, 2024 amesema.
“Saa mbili asubuhi Julai 3, nikampigia tena simu na kumtumia meseji simu zake zikawa hazipatikani, ilibidi nimtafute mshenga nimweleze nampigia mwenzangu simu simpati; alimfuatilia na alipoona hapatikani aliwapigia ndugu zake wa nyumbani kwao Shinyanga kama wamemuona wakasema hawajamuona na simu zake hazipatikani.”
“Baada ya hapo nilimtafuta mtu ambaye anaweza kwenda nyumbani kwake asubuhi, alipofika hakumpata na hata wapangaji waliokuwapo walisema hawajamuona, hata walipogonga mlango hakuna aliyeitika na walipochungulia dirishani hawakuona mtu,” amesema.
Neema amesema baadaye alimuomba dada yake anayefanya kazi KCMC amwangalie kama yupo ofisini kwake ambako alielezwa hajafika kazini na simu zake hazipatikani.
Amesema Masunga ni mchumba wake wa siku nyingi na walifikia hatua ya kumtolea mahari ili taratibu za ndoa zianze.
“Lenga ni mchumba wangu ambaye tulikuwa tumeshatambulishana nyumbani kwa wazazi, mwezi huu wa saba ilikuwa anitolee mahari ili mambo mengine ya ndoa yaendelee,” amesema akibubujikwa machozi.
Amesema kutoweka kwa mchumba wake kumempa mshtuko kwa kuwa tangu amemfahamu hakuwahi kumueleza au kusikia changamoto wala ugomvi wa yeye na mtu mwingine.
“Hapa nilipo najihisi vibaya, mshituko wa kupotea kwake umeniumiza, kibaya zaidi simu zake hazipatikani. Nimeumia, natamani kusikia amepatikana walau nisikie sauti yake, nizungumze naye anieleze kilichomsibu. Naomba Serikali inisaidie kumtafuta,” amesema.
Paschal Jeremiah, kaka wa Masunga amesema bado wanaendelea kumtafuta wakiamini watampata akiwa salama.
“Bado nipo Moshi naendelea kumtafuta mdogo wangu maana simu zake hazipatikani mpaka sasa. Tunaomba Serikali itusaidie akipatikana tutashukuru sana,” amesema.
Kwa mujibu wa taarifa, tukio hilo limeripotiwa Kituo cha Polisi Longuo na kutolewa RB namba LNG/RB/33/2024 na uchunguzi unaendelea.