Agosti 1906, mwandishi wa Marekani, Ida Tarbell, alikamilisha mfululizo wa makala ambayo aliyapa kichwa “John D Rockefeller: A Character Study”, kwa Kiswahili unaweza kuiweka hivi, “John D Rockefeller: Somo la Uhusika.” Nakala ya kwanza ilitoka mwaka 1905 kwenye Jarida la McClure.
Ida, katika makala hayo, alifichua jinsi bilionea huyo wa Standard Oil, alivyokuwa akihusika na biashara za siri na haramu. Kingine, Ida alikwenda mbali na kusimulia kuhusu William Avery Rockefeller, baba mzazi wa John D, alivyokuwa akijihusisha na utapeli katika nyakati zake. Mantiki ya ukumbusho wa makala ya Ida kuhusu John D, tajiri namba moja ulimwenguni nusu ya kwanza ya Karne ya 20, ni dhana jinsi Serikali ya Marekani ilivyoshughulika naye. Ni tajiri, bilionea mkubwa, mmoja wa matajiri wakubwa wa muda wote ulimwenguni, lakini sehemu kubwa ya fedha zake ni chafu.
Je, Serikali ya Marekani itaifishe fedha za John D na kumfilisi kwa kuwa zilikuwa chafu? Matokeo yake yangekuwaje? Mabilioni ya fedha yakiwa kwenye mzunguko, yanachochea faida nyingi; kujenga uchumi wa nchi, kuwezesha makusanyo ya kodi na kukuza ajira.
Uamuzi ambao ulifanywa kwa siri na Serikali ya Marekani ni kumsamehe John D, lakini kwa sharti la kuyatoa gizani mabilioni yake haramu aliyoyatengeneza katika biashara za siri, na kuyaingiza kwenye mzunguko halali. Serikali ya Marekani ilifanya hivyo kwa kuzingatia faida za kila upande, vilevile masilahi mapana ya taifa lao. Nimetangulia na simulizi ya bilionea John D ili isaidie kujenga mantiki katika kujadili tafakuri nyuma ya vifo vya mabilionea wa Tanzania ndani ya miaka mitano iliyopita. Kwa zaidi ya muongo mmoja, mabilionea hao walikuwemo ndani ya 10 bora ya watu matajiri zaidi Tanzania.
Juni 29, 2024, alifariki dunia Yusuf Manji. Machi 23, 2024, bilionea Mustafa Sabodo, alivuta pumzi ya mwisho. Desemba 15, 2020, Subash Patel, alifumba macho jumla. Mei 2, 2019, Reginald Mengi, aliyaanza maisha baada ya kifo. Desemba 8, 2019, Ali Mufuruki, aliipa kisogo dunia ghafla.
Wafanyabiashara hao watano, ndani ya miongo miwili iliyopita, mara zote ilipotajwa orodha ya matajiri 10 Tanzania, ungewakuta. Katika kipindi hicho, walikuwa taswira ya sekta binafsi Tanzania. Biashara zao zilitengeneza ajira kwa Watanzania wengi. Walikuwa kwenye tabaka la walipakodi wakubwa Tanzania. Mzunguko wa biashara zao ulijenga na kuimarisha uchumi wa nchi.
Inafahamika kuwa wengi wao biashara zao zinaendelea kuendeshwa na familia zao au menejimenti zilizokasimishwa. Manji, kwa sehemu kubwa alikuwa ameshahamisha biashara zake, baada ya matukio makubwa ambayo alikutana nayo kati ya mwaka 2017 na 2018.
Kufanya hoja ieleweke vizuri, hasa kutoka kwa mfano wa John D ni kuwa mabilionea wakubwa kupitia biashara zao, kwa kawaida ni washirika wa Serikali katika nyanja muhimu ambazo nimeshazitaja.
Serikali inahitaji kodi kuendesha nchi, kwa hiyo ingetamani kuwa na wafanyabiashara wakubwa kwa wingi ili kufikia malengo ya kibajeti. Serikali inahitaji kugawa ajira kwa wingi ili kudhibiti utitiri wa watu wasio na ajira mitaani. Mabilionea ndio huajiri namba kubwa ya wafanyakazi. Serikali inahitaji kuona mzunguko wa fedha ni mkubwa, na hilo hurahisishwa na mabilionea kupitia mizunguko yao ya biashara na huduma.
Mfano mmoja, Manji peke yake kupitia biashara zake na huduma chini ya kampuni za Quality Group Limited, inakadiriwa kuwa alikuwa ameajiri watu zaidi ya 25,000 hadi mwaka 2017.
Hizo ni ajira za moja kwa moja. Sasa kokotoa, kila mwajiriwa, weka angalau watu watatu wanaomtegemea.
Atapanda vyombo vya usafiri, mafuta yatanunuliwa. Kila mshahara uliolipwa, ulinufaisha jamii nyingine mtaani. Baada ya misukosuko ambayo Manji alikumbana nayo, hivyo kulazimika kuhamisha biashara zake nje ya nchi, maelfu ya Watanzania walipoteza ajira.
Niliwahi kufanya kazi Quality Group. Nilishuhudia watu wengi wakipoteza ajira kuanzia Februari 2017, baada ya kuanza kufunga biashara moja hadi nyingine.
Yupo mtu anaweza kusema kilichompata Manji ni matokeo ya kutotii sheria za kodi na biashara, ambazo zimetungwa na Bunge.
Sitajifanya wakili wa Manji, kumtetea kuwa hakuwahi kuvunja sheria, bali alikomolewa kwa visasi, la hasha! Badala yake nitauleta mfano wa John D na Serikali ya Marekani.
Hasara ya kumshughulikia John D, ingekuwa kubwa kuliko kumbananisha na kumwelekeza ayaelekeze mabilioni yake kwenye biashara halali. Ndivyo ingewezekana kwa Manji. Laiti, hatua za kumshughulikia zingebeba angalizo la ajira ambazo alikuwa anatoa, mzunguko wa fedha aliokuwa anautengeneza, malipo ya kodi aliyofanya, na jinsi mambo hayo matatu yalivyowezesha kukuza uchumi wa nchi, pengine yaliyotokea yasingetokea.
Manji hayupo tena duniani, je, nchi inatafakari nini kuondoka kwake? Je, mabilionea waliopo wanalindwa vipi ili waendelee kuijenga nchi na kutoa ajira? Makosa makubwa ambayo hufanyika Tanzania ni kumtazama bilionea kwa kuona ule ni utajiri wake. Inatakiwa kumtazama bilionea kila upande wa mzunguko wake wa kibiashara, jinsi fedha zake zinavyonufaisha wengi na nchi.
Sabodo, Subash, Mufuruki na Mengi, nini kimewahi kufanyika kuhakikisha biashara walizokuwa wanaongoza kabla ya vifo vyao, hazifi ili ziendelee kuwa na manufaa kwa nchi? Serikali haipaswi kujielekeza kwenye kusimamia sheria za makusanyo ya kodi na ushuru. Inatakiwa kulea biashara.
Waziri wa Fedha, vilevile Waziri wa Viwanda na Biashara, wanatakiwa kujipa wajibu wa ulezi wa biashara. Hiyo siyo kwa mabilionea wakubwa kama Manji, Mengi, Subash, Sabodo na Mufuruki, bali hata matajiri wa kati (semi rich), vilevile wafanyabishara wadogo.
Haifai kuona wafanyabiashara Kariakoo na kwingine, wanagoma kisa kutokuelewana na Serikali kuhusu kodi. Haipendezi kushuhudia bilionea anafariki dunia, halafu familia yake inaingia kwenye migogoro hadi mahakamani, wakati Serikali ingeweza kuwahi kujenga mwafaka wa kifamilia ili biashara zilizoachwa na marehemu ziendelee kama ilivyokuwa kabla ya kifo chake.