HUENDA Kenya ikanyimwa mikopo baada ya kushushwa hadhi kwenye viwango vya Shirika la Kimataifa la kutathmini Madeni ya Mataifa na Utoaji Mikopo (Moody’s). Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Ripoti ya Moody’s iliyotolewa jana Jumanne imeonyesha kuwa, kutotiwa saini kwa Muswada wa Fedha 2024/25 kumechangia Kenya kushuka viwango na kuwa kati ya nchi zinazoelekea kuelemewa na madeni.
Kwa mujibu wa shirika hilo, inaonekana Kenya haitafanikiwa pakubwa kujiondoa hatarini hata katika mikakati ya kupunguza matumizi ya serikali.
Rais William Ruto aliondoa Muswada wa Fedha 2024 kutokana na wimbi la maandamano lililoshuhudiwa nchini humo kwa kuwa mapendekezo mengi ya ushuru yalikuwa katika muswada huo.
Kati ya sababu ambazo zilisababisha raia, hasa vijana wapinge muswada huo ni ushuru ambao ungeongezwa kwenye ununuzi na matumizi ya magari, kutuma na kutoa pesa na pia bei ya mkate kupanda maradufu.
Moody’s pia imeonya kuwa, huenda Kenya ikashindwa kuyalipa madeni yake na sasa imeorodheshwa miongoni mwa nchi hatari zaidi kupewa mikopo na mashirika ya kimataifa.
Juni mwaka huu shirika hilo lilitoa ripoti iliyoweka Ghana pabaya katika kuyalipa madeni yake. Nchi hiyo hatimaye ilielemewa kabisa na sasa inashiriki mikakati ya kubana matumizi yake kulipa madeni mengi yanayoiandama.
Baada ya muswada wa fedha kuondolewa, serikali ya Kenya imeamua kupunguza malengo yake ya mapato ya ushuru mwaka wa fedha wa 2024/25 kwa KSh177 bilioni. Mbali na hayo, pia imetangaza kuwa itapunguza matumizi katika ofisi na idara mbalimbali za serikali kuanzia ofisi ya Rais.
“Kushuka kwa nafasi ya Kenya kunaonyesha nchi haina uwezo wa kuyakusanya mapato ya kutosha ya kulipa madeni yake. Kwa hivyo, Kenya itakuwa ikitatizika sana kulipa madeni hayo kwa sababu ya kutofikia mapato lengwa,” ilisema taarifa ya Shirika la Moody’s Jumanne.
Shirika hilo lilisema kuwa, kupunguza matumizi hakutasaidia kwa sababu kiasi kikubwa cha ushuru kinaelekezwa katika kuyalipa madeni na hilo ni jambo ambalo haliwezi kuepukwa kwa sasa.
“Serikali ya Kenya kwa sasa imepandishiwa gharama ya kupokea mikopo na kuwekewa masharti makali kabla ya kupewa mikopo,” imeongeza taarifa hiyo.
Takwimu kutoka Benki Kuu ya Kenya zinaonyesha kuwa, deni la Kenya sasa limefikia KSh10 trilioni ambalo huchukua zaidi ya asilimia 70 ya mapato ya nchi.
Utawala wa Rais Ruto umekashifiwa kwa kuendelea kukopa fedha licha ya kiongozi huyo wa nchi alipochukua usukani kusema alikuwa akilenga kukwepa mkondo wa kukopa kiholela.
Kwa muda wa miezi minane pekee baada ya kuchukua uongozi wa nchi, utawala wa Kenya Kwanza ulikopa KSh1.2 trilioni.
Katika mwaka wake wa kwanza baada ya kutwaa uongozi mwaka 2013, utawala wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ulikopa KSh874.5 bilioni.
Alipokuwa akiondoka ofisini, Kenya ilikuwa na deni la KSh8.7 trilioni na ikilinganishwa na kiwango cha sasa cha KSh11.2 trilioni. Rais Ruto amekopa KSh2.5 trilioni ndani ya miaka miwili pekee ambayo amekuwa uongozini.
Deni la taifa limekuwa likipaa tangu 2013 kwa kuwa Rais wa tatu marehemu Mwai Kibaki alipoondoka ofisini mnamo 2013, aliacha Kenya ikiwa na deni la KSh1.8 trilioni pekee.
Kwa mujibu wa data kutoka Benki Kuu (CBK) asilimia 73 ya deni la Kenya italipwa kwa Benki ya Dunia, Uchina, Benki ya AFB, Eurobond ambazo zinadai Kenya jumla ya KSh3.97 trilioni. China ndiyo inayoidai Kenya hela nyingi zaidi linalofikia KSh1 trilioni.