Madereva 25 kuchuana Tanga | Mwanaspoti

IDADI ya madereva na waongozaji inatarajiwa kuongezeka maradufu na kufikia 25 wakati mpango wa kuwashirikisha madereva zaidi kutoka Kenya ukiendelea kabla ya mbio hizo kutimua vumbi mkoani Tanga, Julai 21, mwaka huu.

Kwa mujibu wa waandaaji wa mbio hizo, Mount Usambara Club, awali ni madereva 15 pekee walithibitisha kushiriki mbio hizo, lakini idadi hiyo sasa inazidi kuongezea hadi kufikia Julai 20, siku ya mwisho kujisajili.

Akifafanua, Mwenyekiti wa klabu ya Mount Usambara, Hussein Moor alidai kuna madereva wengine 12 walioonyesha dhamira ya kuja Tanga kushiriki mbio hizo zenye kauli mbiu ya ‘Advent Construction Rally of Tanga’.

“Hadi kufikia juma hili watu zaidi ya 12 wameonyesha nia ya kushiriki mbio za magari mkoani hapa, lakini uthibitisho kamili ni pale watakapokamilisha taratibu zote na magari yao kukaguliwa na kupasishwa kwa mashindano baada ya kukidhi vigezo vya usalama (safety,” alisema mwenyekiti huyo.

Miongoni mwa madereva waongozaji (navigators) wa kwanza kuthibitisha ni pamoja na Mzambia, David Sihoka na Awadh Bafadhil ambao ni waongozaji wazoefu barani Afrika.

Sihoka atakuwa akimwongoza dereva Gurpal Sandhu wa Arusha ndani ya gari aina ya Mitsubishi Evo 10 wakati Bafadhil atakuwa akimwongoza dereva kutoka Tanga, Jamal Nirmal Utu.

Moor alisema mbio za mwaka huu zitafanyika katika maeneo ya Pongwe, Mkanyageni na Mlamleni kwani barabara zake ni nzuri kwa madereva kuonyesha ustadi wao katika kona na maeneo ya vumbi jekundu.

Orodha ya madereva gwiji wa Tanzania ambao walikuwa wa kwanza kuthibitisha ushiriki wao ni Randeep Birdi Sunny  kutoka Dar es Salaam na ndugu yake Manvir Birdi ambao wataendesha gari aina ya Mitsubishi Evo 9.

Wengine Aliasger Fazal, Akida Machai, Shaneabas Fazal na Jamal Nirmal wote kutoka Tanga.

Kutoka Morogoro ni dereva mpya Waleed Nahdi ambaye  ataendesha gari aina ya Ford Proto.

Related Posts