Viongozi wanachama wa NATO pia watazungumzia jinsi ya kuimarisha umoja wao kutokana na changamoto zinazouandama ulimwengu wa Magharibi.
Mkutano huo wa kilele unafanyika baada ya sherehe zilizofanyika usiku wa kuamkia Jumatano kuadhimisha miaka 75 tangu kuanzishwa kwa muungano huo wa kijeshi, zilizofanyika mjini Washington.
Rais Biden ahimiza mshikamano
Rais wa Marekekani, Joe Biden ambaye ndiye mwenyeji wa mkutano huo anadhamiria kuhimiza kuhusu mshikamano na ushirikiano usioyumba miongoni mwa wanachama wa NATO pamoja na kuwahakikishia wapiga kura wa Marekani kwamba bado ana uwezo wa kuongoza kwa muhula wa pili madarakani.
Viongozi hao wanatarajia kujadili pia mpango wa Katibu Mkuu wa NATO anayemaliza muda wake, Jens Stoltenberg, wa kuipatia Ukraine msaada wa kijeshi wenye thamani ya euro bilioni 40, ifikapo mwaka 2025.
Stoltenberg amesema matokeo ya vita dhidi ya Urusi yatatoa mwelekeo wa usalama wa kimataifa kwa miongo kadhaa ijayo. Kulingana na Stoltenberg, NATO inahitaji kuishawishi Urusi kwamba haiwezi kushinda vita vyake dhidi ya Ukraine, kwa kusubiri kusitishwa kwa msaada kutoka nchi za Magharibi, hivyo hawawezi kuiacha Urusi ishinde.
NATO: Ni muda wa kusimamia demokrasia na uhuru
“Ukweli ni kwamba hakuna njia mbadala usio na gharama kwa uchokozi wa Urusi kama Jirani. Hakuna njia isiyo ya hatari katika vita. Na kumbuka, gharama kubwa na hatari kubwa zaidi itakuwa kuiacha Urusi kuishinda Ukraine. Hatuwezi kuruhusu hilo litokee,” alifafanua Stoltenberg.
Kiongozi huyo wa NATO amesisitiza kuwa muda wa kusimama imara kwa ajili ya uhuru na demokrasia ni sasa. Wanachama wa NATO wameiunga mkono kwa dhati Ukraine, tangu Urusi ilipoivamia nchi hiyo Februari mwaka 2022.
Rais Biden siku ya Jumanne aliufungua mkutano huo kwa kutangaza kuwa washirika wa NATO watatoa mifumo zaidi ya ulinzi wa anga kwa Ukraine.
Rais wa Ukraine, Volodomyr Zelensky, ambaye pia anahudhuria mkutano huo, ana matumaini kwamba mkutano wa viongozi wa nchi 32 wanachama wa NATO utafafanua matarajio ya uwanachama wa Ukraine katika muungano huo wa kijeshi.
Marekani na Ujerumani kikwazo
Duru za kidiplomasia kutoka ndani ya NATO zinaeleza kuwa Marekani na Ujerumani ndiyo wapinzani wakuu wa kutaka Ukraine kujiunga na jumuiya hiyo hivi karibuni.
Viongozi wa NATO pia wanatarajiwa kujadili changamoto zinazosababishwa na China kutokana na msaada wake wa vifaa vya kivita kwa Urusi, huku Stoltenberg akiielezea China kama mwezeshaji mkuu wa vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.
Viongozi wa Australia, Japan, New Zealand na Korea Kusini, ni miongoni mwa wale walioalikwa kuhudhuria mkutano huo, na wako Washington kwa ajili ya kuimarisha uhusiano na NATO.
(AFP, DPA, Reuters)