Mmoja kati ya watatu ana shinikizo la juu la damu

Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema theluthi moja ya watu wazima duniani wana shinikizo la juu la damu, sawa na mtu mmoja kati ya watatu.

Takwimu hizo za WHO kwa mujibu wa wataalamu, zinawiana na hali ilivyo nchini Tanzania, hivyo wameshauri mambo saba ya kuzingatiwa kuepuka au kukabiliana na tatizo hilo.

Miongoni mwa hayo ni kupima afya mara kwa mara, kupunguza matumizi ya chumvi, kuacha uvutaji wa sigara, kulala ipasavyo kwa muda unaotakiwa na kuepuka msongo wa mawazo.

Akizungumza na Mwananchi leo Julai 10, 2024, Mkuu wa Kitengo cha Utafiti katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Pedro Palangyo amesema takwimu za WHO zinawiana sawia na hali halisi nchini pamoja na wagonjwa wanaoonwa katika taasisi hiyo.

“Theluthi moja ya watu duniani wana shinikizo la juu la damu. Hali kwetu iko vivyo hivyo, kwenye jamii asilimia ni hiyohiyo. Kwenye Taasisi ya Moyo takribani robo tatu ya wagonjwa wote tunaowaona wana shinikizo la juu la damu,” amesema Dk Palangyo ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo hospitalini hapo.

Kutokana na hali hiyo, Daktari mshauri mwandamizi magonjwa ya ndani na maradhi ya moyo JKCI, Profesa Harun Nyagori amesema kuna umuhimu kwa jamii kuchunguza afya kwani kuna visababishi vingi na walio na shinikizo la damu kutofahamu hali zao mapema.

“Tatizo la shinikizo la damu linaweza kukupata na isionyeshe dalili yoyote kwa walio wengi, tatizo ni kubwa kwa kuwa wengi hawatambui hali zao, wanapogundulika tayari madhara ni makubwa. Mfano, unakuta tayari mtu ana kisukari, mshtuko wa moyo na matatizo ya figo kushindwa kufanya kazi,” amesema.

Profesa Nyagori amesema wengi wa wagonjwa kutotumia dawa kwa maelekezo sahihi na wengine kusitisha dawa kabla ya kupewa maelekezo na wataalamu ni changamoto kubwa.

Ametaja changamoto nyingine ni kuwa wapo wasiofuata maelekezo ya chakula, kuongeza chumvi mezani, utumiaji mkubwa wa pombe kali na kwa kiwango kikubwa, msongo wa mawazo na kukataa kufanya mazoezi rahisi yanayoelekezwa.

“Wengine ni kutoamini kuwa anaumwa au shinikizo la damu linaweza likamletea madhara makubwa, na wengine kuamini imani za kishirikina au potofu na kukataa kupata uchunguzi na matibabu sahihi,” amesema Profesa Nyagori.

Takwimu katika tovuti ya WHO zinaonyesha takribani watu wazima zaidi bilioni 1 wenye umri wa miaka 30 hadi 79 duniani wana shinikizo la juu la damu, wengi wao (theluthi mbili) wanaishi katika nchi za kipato cha chini na cha kati.

Ofisa wa kitengo cha magonjwa ya moyo na mishipa wa WHO, Dk Tasekeen Khan ameeleza tatizo hilo ni sababu kuu ya kifo cha mapema duniani, akifafanua kwa nini shinikizo la juu la damu linatambulika kama muuaji wa kimya-kimya.

“Inaitwa ‘silent killer’ kwa sababu huzioni kabisa dalili na ndiyo maana kwa sasa tatizo hili linaathiri mtu mmoja mzima kati ya watatu duniani; na kati ya watu watano wenye shinikizo la juu la damu ni mmoja pekee anayeweza kudhibiti hali hiyo kwa matibabu,” alisema Dk Tasekeen.

Kutokana na hali hiyo, amesema WHO ina mikakati iliyowekwa kuhakikisha inaokoa zaidi ya watu milioni 76 ifikapo mwaka 2050, kwa kutoa elimu na kuendelea kuangalia namna ya kudhibiti changamoto hiyo.

Takwimu zinaonyesha, idadi ya watu wanaoishi na shinikizo la juu la damu iliongezeka kutoka milioni 650 mwaka 1990 na kufikia watu bilioni 1.3 mwaka 2019.

Dk Tasekeen amesema ili kudhibiti shinikizo la juu la damu, kwanza mtu anatakiwa kufuatilia matibabu kwa kupima mara kwa mara na kushauriana na daktari.

“Kama ukibainika na shinikizo la damu, ni muhimu kuanza matibabu mara moja kama ambavyo mwongozo wa WHO unaelekeza,” amesisitiza.

Ametaja vitu vinne vinavyopaswa kufuatwa ili kujikinga na tatizo hilo kuwa ni kuepuka uvutaji wa sigara, chumvi nyingi kwenye chakula au ya kuongeza mezani.

Dk Tasekeen ametaja kulala kwa muda unaotakiwa ni muhimu kwa ajili ya kudhibiti shinikizo la damu, na ni muhimu kupunguza msongo wa mawazo au kuepukana nao.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya moyo, Peter Kisenge amesema mtu anapokaa kwa muda mrefu na tatizo la shinikizo la juu la damu, huzalisha magonjwa mengine yasiyoambukiza kutokana na mfumo mzima wa ugonjwa huo ulivyo.

“Wengi hawajui kama wana presha, ukiona mapigo yako ya moyo yapo kuanzia chini ya 120 kwa 80 hiyo ndiyo presha inayotakiwa. 60 mpaka 80 na 120 mpaka 130 mapigo yako yapo sawa. Ukiona yameshuka zaidi au kupanda zaidi kama 80 kwa 140 unatakiwa kumuona daktari,” amesema.

Dk Kisenge amesema kuna umuhimu wa watu kuwa makini na ulaji chumvi ya kuongeza mezani kwani ni chanzo cha shinikizo la juu la damu ambalo husababisha maradhi ya moyo.

Amesema watu wamekuwa wakitumia chumvi kupita kiasi na hawawezi kuchunguza afya zao mara kwa mara, utamaduni alioutaja kuwa wa hatari kwa afya.

“Duniani wanaojua kuhusu hali zao kwamba wana shinikizo la damu ni asilimia 50 pekee hapa kwetu ni asilimia 10 peke yake, kwa JKCI wagonjwa 10 tunaowaona kwa mara ya kwanza, sita wana shinikizo la damu na hawakutambua hali zao,” amesema.

Dk Kisenge amesema wanaotumia dawa za maisha hasa wanaougua kisukari, moyo, shinikizo la damu na magonjwa mengine wapo hatarini kupata maradhi ya figo.

Kwa wagonjwa wanaotibiwa JKCI, kati ya wagonjwa 83,356 waliotibiwa mwaka 2022 asilimia 66.8 (59,022) walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu.

Hii ina maana kwa kila wagonjwa 10, sita wana tatizo la shinikizo la juu la damu au madhara ya ugonjwa huu.

Takwimu mpya zilizotolewa na Wizara ya Afya mwaka 2023 zilionyesha kuna ongezeko la watu 890,788 sawa na asilimia 3.8 ikilinganishwa na asilimia 3.6 kipindi kama hicho mwaka 2021/22.

Related Posts