Serikali kushirikiana na Misri kibiashara

SERIKALI imesema kuwa itaendelea kushirikiana na nchi ya Misri katika masuala ya biashara ili kuhakikisha wafanyabiashara wanaendelea kupata fursa za kupeleka bidhaa mbalimbali nchini humo.

Akizungumza jana katika Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Misri kwenye Maonesho ya 48 ya biashara ya kimataifa Sabasaba, Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE) Prof. Ulingeta Mbamba alisema kuwa Tanzania ipo kwenye nafasi nzuri ya kupeleka bidhaa za chakula, umeme na biashara zingine nchini humo.

Prof. Mbamba alisema takwimu zinaonesha kuwa Tanzania inapekela bidhaa zenye thamani ya shillingi dola milioni moja, huku Misri zikileta bidhaa nchini Tanzania zenye thamani dola milioni 60.

“Siku ya leo imetoa fursa kwa wafanyabiashara kuonesha nini ambacho wanafanya katika nchi hizo mbili, kwani Tanzania inavitu vingi vya kujifunza na kupeleka Misri ikiwemo masuala ya chakula, vitu vya umeme na biashara nyingine” alisema Profesa Mbamba.

Prof. Mbamba alisema kuwa mikutano ya kibiashara kati ya nchi hizo itaendelea kufanyika ambayo inaendelea kuleta tija katika biashara kati ya nchi hizo.

Balozi wa Misri nchini Tanzania, Shariff Ismail, alisema kuwa kupitia mkutano huo, matunda yataonekana baina ya nchi hizo mbili kupitia ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji katika kukuza uchumi.

Alisema kuwa ni muhimu kwa nchi ya Misri na Tanzania kwani mpaka kufikia sasa tunaadhimisha miaka 60 ya uhusiano , katika historia tunauhisiano imara.

“Kama balozi tunatafuta njia za kuimarisha uhusiano wetu kwa sababu watu wetu na historia yetu inastahili kushirikiana” alisema Ismail.

Meneja Uenezi na Masoko, Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Khamis Dunia alisema kuwa mwamko ni mzuri kwa nchi ya Misri kwani kuna taasisi 36 zimeshiriki katika maonesho ya Sabasaba ya mwaka huu pamoja na sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi, uhandisi na zingine zinazohusiana na uchumi wa bluu.

“Katika maonesha ya sabasaba Zanzibar inatangaza fursa zilizopo katika uchumi wa buluu (bahari na pembezoni mwa bahari) ambazo ni utalii, uvuvi, ukulima wa baharini, usafiri wa bahari, na tapo katika hatua ya kuendelea kutafuta wawekezaji kutoka Misri na ili kuwekeza Zanzibar. ” alisema Dunia.

Related Posts