SERIKALI imesema inaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP) unaoendelea sasa na kuongeza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika kama ulivyopangwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam… (endelea).
Akizunguma baada ya kutembelea banda la EACOP katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema toka mkataba rasmi wa utekelezaji wa mradi huo (-FID) uliposainiwa Februari 2022 jijini Kampala nchini Uganda, mradi huo umekuwa ukienda vizuri kama ilivyopangwa awali.
Amesema kazi zote za awali katika utekelezaji wa mradi huu ukiwemo usanifu na ulipaji fidia kwa waguswa takribani 13,161 zilikwishamalizika na zaidi ya asilimia 99 tayari wamekwishalipwa fidia hiyo.
“Asilimia iliyobaki ni ndogo sana na hawajalipwa kwa sababu mbalimbali ikiwemo zinazohusiana na mirathi,” amesema Mhandisi Mramba na kuongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo utachangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mramba, miongoni mwa kazi zinazoendelea hivi sasa ni pamoja na usambazaji wa mabomba yatakayofukiwa ardhini kwa ajili ya usafirishaji wa mafuta hayo ambapo mabomba hayo yanawekewa mfumo wa kupasha joto mafuta hayo ghafi ili yasafiri kwa urahisi kwa sababu ni mazito.
Amesema kazi hiyo ya kuwekea mabomba hayo mifumo ya upashaji joto mafuta pamoja na plastiki itakayozuia upotevu wa joto mradi inaendelea katika kiwanda kilichopo katika kijiji cha Sojo wilayani Nzega mkoani Tabora.
“Mradi unapiga hatua vizuri sana kama ulivyopanga na Serikali tunafurahia sana maendeleo haya,” amesema na kuongeza kuwa mradi huo umekuwa ukipitia hatua mbalimbali za utekelezaji wake kutokana na ukubwa wake.
Mhandisi Mramba amesema maendeleo yaliyofikiwa hivi sasa, serikali ina mategemeo kuwa mradi huu utamalizika mwishoni mwa 2025 kama ilivyopangwa hapo awali.
Amesema mradi huo una urefu wa jumla ya kilomita 1,443 kati ya hizo kilomita 296 zipo nchini Uganda na kilomita 1,147 zipo Tanzania.
Bomba hilo linapita katika mikoa manane ya Tanzania Bara ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga, likijumuisha wilaya 24, kata 134 na vijiji zaidi ya 180.
EACOP Ltd ni kampuni yenye madhumuni maalum, inayosimamiwa na Mkataba wa Wanahisa wake ambao ni Total Energies wahisa 62, Uganda National Oil Company (UNOC) wahisa 15, Shirika la Maendeleo Tanzania (TPDC) wanahisa 15 na Ksmpuni ya Kichina ya CNOOC wanahisa wanane.