Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Deogratias Ndejembi amewataka wakuu wa mikoa kufanya operesheni na kuwakamata waganga wa jadi wanaofanya shughuli hizo bila vibali.
Amesema lengo ni kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino, vinavyotajwa kuchochewa na ramli chonganishi zinazopigwa na waganga hao.
Agizo la Ndejembi linakuja wiki chache tangu lilipotokea tukio la mauaji ya mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath (2) na tayari watuhumiwa akiwamo mganga wa jadi na baba yake mzazi wameshafikishwa mahakamani.
Ndejembi ametoa maelekezo hayo jana Julai 9, 2024 alipokuwa akizindua kampeni ya kitaifa ya kupinga ukatili dhidi ya watu wenye ualbino iliyoanzia mkoani Kagera.
“Fanyeni operesheni ya kukamata waganga wa tiba asili na mbadala ambao wanafanya shughuli hizo bila vibali vya wizara ya afya na wote wanaojihusisha na ramli chonganishi na wafikishwe kwenye vyombo vya sheria,” amesema.
Hata hivyo, amesema tayari mafuta kwa ajili ya ngozi za wenye ualbino ili kuwakinga na saratani yameshanunuliwa na kutakabidhiwa Wizara ya Afya Julai 13, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Ndejembi, Serikali imetoa Sh1 bilioni kwa mfuko wa watu wenye ulemavu kwa ajili ya kuendeshea vyama vyao.
Sambamba na hayo, amesema mfumo wa usajili wa watu wenye ualbino kielektroniki umeshaanzishwa na hivi karibuni utazinduliwa.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye Ualbino (TAS), Alfred Kapole ameiomba Serikali iongeze juhudi za kuwalinda, badala ya kuacha kazi hiyo kwa Jeshi la Polisi pekee.
Awali, Mkuu wa Mkoa Kagera, Fatma Mwassa amesema mkoa huo una jumla ya watu wenye ualbino 275 kati yao 142 ni wanaume na 133 ni wanawake.
“Mkoa huu una wingi wa watu wenye ualbino na tunaendelea kufanya ulinzi dhidi yao, kama tunavyoelekezwa na Serikali tunasikitika kuona kampeni hii inazinduliwa hapa baada ya mtoto wetu mpendwa Asimwe kuuawa kikatili,” amesema.