Simba tena kwenye makazi ya watu Iringa, mmoja auawa

Iringa. Ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu simba wazue taharuki katika wilaya za Iringa na Kilolo, wanyama hao wameibuka tena katika Wilaya ya Mufindi, mmoja akiuawa na wananchi baada ya kushambulia mifugo.

Diwani wa Igowole, Castory Masangula amesema leo Julai 10, 2024 kuwa wameua simba anayedaiwa kula ng’ombe watano katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo.

Inadaiwa simba mwingine mwenye watoto ametoroka kuelekea msituni katika kata hiyo, jambo linaloelezwa linahatarisha usalama wa wananchi.

Juni, 2023 mifugo kadhaa wakiwamo ng’ombe waliuawa na simba waliovamia makazi ya watu katika vijiji kadhaa vya wilaya za Iringa na Kilolo kabla ya kuuawa.

Akizungumza na Mwananchi, Masangula amesema simba huyo aliuawa usiku wa kuamkia leo Julai 10, 2024 karibu na ilipo Hospitali ya Wilaya ya Mufindi.

Amesema kazi ya kumsaka simba huyo imefanyika kwa ushirikiano na baadhi ya vijana na askari wa maliasili.

“Tumeshirikiana na vijana wanaofanya kazi kwenye Kampuni ya Melab na watu wa maliasili. Tumemuua mmoja mwingine amekimbia tunaendelea kumtafuta,” amesema Masangula.

Amesema simba aliyetoroka inahisiwa kuwa alikuwa na watoto kwa sababu wameona nyayo zao.

“Wananchi wachukue tahadhari kwa sababu simba huyu bado yupo,” amesema diwani huyo.

Baadhi ya wananchi wameiomba Serikali kusaidia kumsaka simba huyo ili kunusuru mifugo yao.

“Tunaomba msaada simba huyo auawe kwa sababu kama atabaki hatari kwetu na mifugo yetu,” amesema Anitha Kilasi, mkazi wa Igowole.

Mwaka jana katika Wilaya ya Kilolo simba walivamia vijiji vya Imalutwa, Kising’a, Lugalo na Ihimbo ambako ng’ombe watatu waliuawa.

Wilayani Iringa ng’ombe 34 waliuawa na simba, kondoo (4), mbuzi (7), nguruwe (7) na kuku mmoja.

Simba wilayani humo walivamia kwenye msitu mkubwa unaotenganisha vijiji vya kising’a na Imalutwa.

Related Posts