TETESI ZA USAJILI BONGO: Mkenya kwenye rada za Yanga

YANGA imeanza mazungumzo na kiungo mshambuliaji Mkenya, Duke Abuya baada ya mkataba wake na Singida Black Stars kuisha.

Nyota huyo aliyejiunga na Singida akitokea timu ya Kenya Police, inaelezwa huenda akatua Jangwani ili kupata changamoto mpya huku Yanga ikiingilia kati dili baada ya awali Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ kumhitaji pia.

UONGOZI wa Yanga huenda ukaachana na mpango wa kumsajili mshambuliaji wa Al-Nasr Benghazi ya Libya. Mghana Jonathan Sowah.

Yanga ilitaka kumsajili mchezaji huyo baada ya kuonyesha uwezo mkubwa wakati timu hiyo ilipokutana na Medeama ya kwao Ghana kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi msimu uliopita ingawa kwa sasa mpango huo umesitishwa.

JKT Tanzania iko katika hatua nzuri ya kuinasa saini ya aliyekuwa beki wa kushoto wa Biashara United, Karimu Bakili ‘Chonto’.

Beki huyo aliyewahi kucheza klabu mbalimbali zikiwemo Kagera Sugar na Mbuni, inaelezwa yupo hatua za mwisho za kujiunga na kikosi hicho msimu ujao huku suala la maslahi binafsi likiwa limefikiwa.

ALIYEKUWA kiungo wa Yanga, Omary Chibada yupo katika mazungumzo ya kujiunga na Kagera Sugar kwa ajili ya msimu ujao.

Kagera inatumia nafasi hii kumnasa mchezaji huyo ambaye kwa sasa yupo huru baada ya kuachana na Pamba Jiji aliyoipandisha Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao huku akiwahi pia kuzichezea timu mbalimbali ikiwemo Biashara United.

Related Posts