Vielelezo vyaibua mvutano mkali kesi ya ukahaba

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inatarajia kuwa na mashahidi 15 na vielelezo 10 katika kesi ya kufanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara inayomkabili Amina Ramadhani na wenzake 17.

Mashahidi hao wanatarajia kutoa ushahidi wao, Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive, Dar es Salaam baada ya upelelezi wa shauri hilo kukamilika na washtakiwa kusomewa hoja za awali (PH).

Wakili wa Serikali, Regina Kanyuni akisaidiana na Winifrida Wiko, ameieleza Mahakama hiyo leo Jumatano, Julai 10, 2024 wakati akiwasomea maelezo hayo, mbele ya Hakimu Mkazi, Francis Mhina.

Washtakiwa hao wanatetewa na mawakili Peter Madeleka, Gaston Garubindi na Maria Mushi.

Akiwasomea maelezo hayo, wakili Kanyuni alidai kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi jinai 17279 ya mwaka 2024, yenye shtaka moja la kufanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa ajili ya kufanya umalaya kinyume na kifungu cha 176 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Amedai washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Juni 14, 2024 maeneo ya Sinza Mori, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja, walikutwa wakifanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa kusimama hadharani, wakiwa wamevaa mavazi yasiyo ya heshima kwa lengo la kufanya umalaya.

“Washtakiwa walikutwa wakiwa wamevaa mavazi yasiyokuwa ya kujistiri, mavazi ambayo yalikuwa yanaonyesha maungo yao walikuwa wamesimama maeneo ya umma kwa lengo la kufanya ukahaba,” amedai wakili Kanyuni.

Wakili huyo ameendelea kudai washtakiwa wakiwa eneo hilo walikamatwa askari polisi na kupelekwa Kituo cha Polisi Mburahati kwa ajili ya mahojiano.

Baada ya mahojino polisi, Juni 24, 2024 washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa shtaka lao.

Washtakiwa baada ya kusomewa shtaka hilo, walikubali majina yao na taarifa binafsi huku wakikana shtaka hilo.

“Mheshimiwa hakimu, upande wa mashtaka tunatarajia kuwa na mashahidi 15 na kwa upande wa vielelezo tunaomba tuvihifadhi, tusiviorodheshe kwasasa,” amedai wakili Kanyuni.

Madeleka apinga ombi la Serikali

Madeleka amepinga ombi la upande wa mashtaka la kutotaja idadi ya vielelezo na kuomba Mahakama itoe amri upande wa mashtaka utaje idadi ya vielelezo kwa kuwa sio siri.

“Naomba Mahakama isikubaliane na hoja ya upande wa mashtaka ya kutaka kuzuia kujata idadi ya vielelezo, hivyo sisi tunaomba iwaelekeze wataje idadi ya vielelezo watakavyotumia katika kesi hii na isiwe suala la kushtukizana,” amedai wakili Madeleka.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mhina ametoa uamuzi kwa kuelekeza upande wa mashtaka kutaja idadi ya vielelezo hivyo huku akiweka bayana kuwa kesi hiyo sio kesi ya hatari kiasi kwamba upande wa mashtaka wapate hofu ya kuvitaja.

“Nakubaliana, Katiba lazima ifuatwe na msingi wa kuwasomea hoja za awali washtakiwa hao ni kufanya kesi hii ianze kusikilizwa kwa haraka, hivyo ni jukumu letu sote kufuata Katiba ya nchi na msingi wa kusimamia haki,” amesema Hakimu Mhina.

“Ninaona hoja ya upande wa utetezi ina mashiko na upande wa mashtaka mnawajibu wa kutaja idadi ya vielelezo,” amesema Hakimu Mhina.

Hakimu Mhina baada ya kutoa uamua huo, Wakili Kanyuni ameiomba Mahakama tarehe itakayopanga kwa ajili ya kuanza usikilizwaji wa shauri hilo ndio siku watakayo taja majina ya vielelezo hivyo.

“Kwa kuwa kesi hii inaendeshwa na mawakili wengine, naomba Mahakama iridhie tuende tukajadiliane na wenzetu na tarehe itakayopangwa, kabla ya kuanza kusikiliza shauri hili tutataja idaidi ya vielelezo,” amedai wakili Kanyuni.

Hata hivyo, wakili Madeleka amepinga tena ombi hilo na kudai iwapo upande wa mashtaka hawajakubaliana na amri iliyotolewa waseme au wapinge na sio vinginevyo.

“Mheshimiwa hakimu, naomba upande wa mashtaka watekeleze amri iliyotolewa na Mahakama ili tuweze kuendelea na hatua nyingine, na kama hawajakubaliana na amri uliyotoa, basi waseme au wapinge na sio kutuambia tusubiri mpaka terehe ya kuanza kusikiliza kesi, hatutaki kushtukizana,’’ amedia Madeleka.

Baada ya mvutano mkali baina ya upande wa mashtaka na upande wa utetezi, upande wa mashtaka walikubaliana na amri ya Mahakama na kutaja idadi ya vielelezo ambavyo ni 10.

“Upande wa mashtaka tunatarajia kuwa na vielelezo 10,” amedai wakili Kanyuni.

Hakimu Mhina baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 29, 2024 kwa ajili ya kuanza kusikilizwa huku akisisitiza upande wa mashtaka kwa siku hiyo wapeleke mashahidi wasiopungua watatu na washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana.

Related Posts