Rais Biden amesema Ukraine iliyokumbwa na vita inahitaji msaada zaidi na ameapa kuilinda Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Katika hotuba yake aliyoitoa siku ya Jumanne, Biden alisema NATO ilikuwa na nguvu kuliko ilivyowahi kuwa hapo kabla na kwamba Ukraine inaweza na itamzuia Rais wa Urusi Vladimir Putin, ikiwa itaungwa mkono kikamilifu na kwa pamoja.
Kuidhinishwa kwa msaada zaidi
Aidha, Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg amesema anatarajia kuwa washirika wa NATO wataidhinisha msaada wa kutosha kwa Ukraine ili kuisaidia katika vita vyake na Urusi na watatanua ushirikiano mwingine katika eneo la Asia na Pasifiki.
”Pia tutafanya maamuzi muhimu kwa ajili ya siku zijazo. Kuhusu matukio yanayoendelea Ukraine na jinsi ya kutanua ushirikiano wetu, hasa na washirika wetu wa eneo la Asia na Pasifiki. Kuhusu Ukraine, ninatarajia washirika watakubaliana kuidhinisha awamu nyingine ya msaada ambao utakuwa na vipengele vitano,” alibainisha Stoltenberg wakati akizungumza na waandishi habari.
Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amesisitiza umuhimu wa msaada wa NATO kwa Ukraine, akisema kila nchi mwanachama italazimika kufanya kila iwezalo na kutambua jukumu maalum kwa Ujerumani kama mwanachama mkubwa zaidi wa Ulaya katika muungano huo wa kijeshi.
Akizungumza leo Jumatano pembezoni mwa mkutano wa kilele wa viongozi wa NATO, Scholz amesema Ujerumani ni nchi kubwa zaidi ya Ulaya ndani ya jumuia ya NATO. Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Ujerumani, hilo linawapa jukumu maalum la kipekee sana, na kwamba watatimiza wajibu huo.
NATO: Ukraine iko kwenye njia thabiti
Ama kwa upande mwingine, Stoltenberg amesema ni mapema mno kusema ni lini Ukraine itakuwa mwanachama wa jumuiya hiyo, lakini iko kwenye njia thabiti kuelekea lengo hilo. Amesema anatarajia Marekani itabakia kuwa ‘mshirika thabiti’ bila kujali matokeo ya uchaguzi.
Huku hayo yakijiri, Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani Antony Blinken, amesema washirika wa NATO wameanza kutekeleza ahadi yao ya kuipatia Ukraine ndege za kivita chapa F-16, ili kuimarisha ulinzi dhidi ya mashambulizi ya Urusi. Blinken amesema ndege hizo zinapelekwa kutoka Denmark na Uholanzi.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amezishukuru Marekani, Denmark na Uholanzi kwa kuimarisha vikosi vya anga vya nchi yake. Shukrani hizo amezitoa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X.
Soma Zaidi: Viongozi wa NATO wakutana Marekani
Wakati huo huo, washirika wa NATO wamefikia makubaliano kuhusu tamko la mkutano huo wa kilele ambalo linajumuisha ahadi ya muungano huo wa kijeshi kuendelea kuisaidia Ukraine, ikiwemo nchi hiyo kuwa mwanachama wa NATO.
Kulingana na duru za NATO, tamko hilo linaendelea kuthibitisha kwamba NATO “itakuwa katika nafasi ya kutoa mwaliko kwa Ukraine kujiunga na jumuiya hiyo wakati washirika watakapokubali na masharti yote yatakapoweza kutekelezwa.