VITAMBULISHO VYA TAIFA KUWAFUNGULIA FURSA WANANCHI WA KIGOMA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kalinzi akiwa ziarani Mkoa wa Kigoma tarehe 09 Julai 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na wananchi wa Mnanila akiwa ziarani Mkoa wa Kigoma tarehe 09 Julai 2024.

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema tayari maelekezo yametolewa kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhakikisha inaharakisha upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa ili kuondoa adha wanayopitia wananchi wa Kigoma na maeneo mbalimbali nchini.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa eneo la Mnanila akiwa ziarani mkoani Kigoma. Amesema kukosekana kwa vitambulisho hivyo kunawanyima fursa mbalimbali wananchi hao ikiwemo kukosa ajira katika miradi inayotekelezwa mkoani humo.

Makamu wa Rais ameusisitiza uongozi wa Mkoa wa Kigoma kushughulikia changamoto ya kukataliwa kupata ajira za kawaida katika mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa sababu ya ukosefu wa vitambulisho vya Taifa. Amesema suala hilo linapaswa kushughulikiwa kwa wananchi kupata ajira hizo kwa kutumia vitambulisho mbadala kama vile leseni na vitambulisho vya kupigia kura. Ameongeza kwamba wananchi wataweza kulinda vema miradi hiyo kama watashiriki katika ujenzi wake.

Amewahakikisha wananchi wa eneo hilo kwamba serikali italipa fidia kwa madai halali ya wote waliochukuliwa maeneo yao kwaajili ya ujenzi wa forodha.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amezungumza na wananchi wa Kijiji cha Kalinzi kilichopo Wilaya ya Kigoma ambapo amewasihi kulinda na kutunza amani iliyopo nchini. Amewasihi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa ili kuhakikisha wanachagua viongozi bora watakaowatumikia vema.

Pia amewahimiza kufanya kazi kwa bidii pamoja na kulinda na kuhifadhi mazingira.

Vilevile Makamu wa Rais amezungumza na wananchi wa Wilaya ya Buhigwe ambapo amewahakikishia kwamba Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya mkoa wa Kigoma ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli za kiuchumi kirahisi ikiwemo biashara.

Amesema adha iliyowakabili wananchi kwa muda mrefu ya ukosefu wa miundombinu bora inakaribia kumalizwa kabisa na serikali ya Awamu ya Sita. Aidha amewaeleza wananchi hao dhamira ya serikali katika kuufungua mkoa wa Kigoma kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vituo vya kupooza umeme Nguruka pamoja na Kidahwe ambavyo vitawezesha mkoa wote wa Kigoma kuanza kutumia umeme wa gridi ya Taifa.

Makamu wa Rais amesema serikali inaendelea kutekeleza kikamilifu miradi ya ujenzi wa barabara kiwango cha lami ili kuunganisha mkoa huo na mikoa mingine ya Tanzania ambapo kwa upande wa barabara ya Tabora – Kigoma ni kilometa 51.1 pekee zimesalia kukamilika na zinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Machi 2024. Pia amesema kwa upande wa barabara ya Kagera – Kigoma ni kilometa 16 pekee zimesalia kuunganisha mikoa hiyo.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema kukamilika kwa uwanja wa ndege wa kisasa unaojengwa mkoani Kigoma kutafungua fursa ya utalii na biashara mkoani humo. Pia amesema Mkoa huo unatarajiwa kuondokana na changamoto ya kufuata huduma za afya katika maeneo mengine ya nchi kwa kuwa serikali inatarajia kujenga Hospitali ya Kanda ya Magharibi katika eneo la Ujiji mkoani humo.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba Mkoa wa Kigoma unatarajia uwepo wa Chuo Kikuu cha masuala ya afya kutokana na mradi wa ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya Muhimbili (MUHAS) katika eneo la Ujiji mkoani humo.

Makamu wa Rais amewahimiza wananchi wa Buhigwe kuzingatia katika kuhakikisha watoto wanapata elimu kwa kuwa serikali imerahisisha suala hilo kwa kutoa elimu bila ada kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita. Pia amewasihi kuwafuatilia watoto mashuleni wanayojifunza ili kukabiliana na wimbi la elimu isiyofaa kwa maadili ya kitanzania.

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa amewaahidi wananchi wa Kigoma kuwakabidhi barabara ya Kasulu – Buhigwe hadi Manyovu (KM 68.25) na barabara ya Kasulu Kibondo (KM 16) ifikapo mwezi Machi 2025 ili kurahisisha shughuli za kibiashara na uwekezaji mkoa wa Kigoma.

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

10 Julai 2024

Kigoma.

Related Posts