Dar es Salaam. Wananchi, wadau na wanaharakati wa haki za binadamu nchini Tanzania, wameeleza chanzo cha watu wanaodaiwa kupotea au kutekwa huku wakitaja suluhisho la kuondokana na vitendo hivyo nchini.
Wamesema suala la ushirikina, visasi au kuzima harakati za kundi fulani linaloonekana kuwa mbele kuhamasisha watu kudai haki fulani ni miongoni mwa vyanzo vinavyodaiwa kusababisha hali hiyo.
Hata hivyo, ili kuondokana na hali hiyo, wamependekeza vyombo vya dola kutimiza majukumu yake, kuunda tume ya kijaji kuchunguza matukio hayo, kuwalinda wanaotoa taarifa za vitendo hivyo.
Wameeleza hayo leo Jumatano Julai 10, 2024 wakati wakichangia mjadala wa Mwananchi X Space (zamani Twitter) uliokuwa na mada ya “Kuongezeka madai ya watu kupotea kutekwa nchini, nini chanzo, suluhisho?”
Kwa nyakati tofauti, Mwananchi imekuwa ikiripoti habari za watu wanaodaiwa kutekwa, ikiwamo tukio la mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam Edgar Mwakabela ‘Sativa’ aliyetoweka Juni 23, 2024 na kupatikana Juni 27 katika Pori la Hifadhi ya Katavi akiwa na majeraha mwili.
Ukiacha suala la Sativa tukio jingine ni la Kombo Mbwana kada wa Chadema wilayani Handeni mkoani Tanga, aliyetoweka Juni 29, mwaka huu hadi sasa bado hajaonekana.
Inadaiwa Mbwana alifuatwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake na kumchukua kinguvu.
Hata hivyo, Julai 3 2024 Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alisema Tanzania iko salama na vitendo vya utekaji havipaswi kukaliwa kimya, akirejea chapisho la Gazeti la Mwananchi la Julai 2,2024 lililokuwa na kichwa cha habari: Nani mtekaji?
“Nadhani mmesoma gazeti moja la Mwananchi limeandika utekwaji, taharuki kubwa inazushwa katika jamii, kwamba Tanzania kuna kutekwa hovyo, niwahakikishie tu Tanzania, iko salama,” alisema Waziri Masauni.
Akizungumza katika mjadala huo, Mhariri wa Dawati la Siasa wa Mwananchi, Peter Elias amesema ni jambo la kusikitisha kuona Watanzania wakitoweka akidai hakuna maelezo yanayojitolesheleza kutoka katika kwa mamlaka husika.
Elias amedai hali hiyo haijazoeleka hapa nchini, akisisitiza mfululizo wa watu kudaiwa kutekwa au kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
“Hili ni suala lina sura nyingi, kisiasa, watu kulipa visasi au vitendo vya ushirikina ni suala mtambuka, linalotakiwa kufanyiwa kazi. Lakini chanzo kikubwa ni mmomonyoko wa maadili, maana Watanzania tuna maadili na tunaishi pamoja, sasa yakitokea mambo kama haya tunaonekana tunakiuka misingi iliyoasisiwa.
“Suluhisho ni vyombo vya dola kutekeleza majukumu yao kikamilifu ili kuwaondoa hofu wanajamii ili wawe sawa na kuishi kwa amani na utulivu, sifa inayojivunia Tanzania,”amesema Elias.
Elias amewataka Watanzania kujenga ustaarabu katika masuala ya kutolipa kisasi na kutumia vitendo vya ushirikina kwa kufanikisha jambo fulani,”amesema.
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa amesema kuna aina mbili za utekaji ikiwamo unaohusisha wananchi kwa wananchi na unaowakumba wanaharakati, wanahabari na wanasiasa.
“Unapozungumzia utekeji ni dhana iliyopo kwa muda mrefu kuna watu wakitekwa wanadai fedha au wengine wanawateka mahasimu wao ili kuwakomoa au kudai vitu fulani. Katika matukio yanayohusisha wananchi kwa wananchi, kumekuwa na jitihada za kuyakomesha.
“Lakini matukio yanayodaiwa kuhusishwa vyombo vya dola ni matukio yanayokuja kwa malengo kadhaa ikiwamo kutia hofu au wananchi wasiendelee kudai au kusimamia msimamo fulani,” amesema Ole Ngurumwa.
“Tunaomba viongozi wetu kuridhia mkataba wa kimataifa kuhusu ulinzi wa watu wote dhidi ya utekaji na upoteaji wa kulazimishwa. Ndani ya mikataba hiyo kuna sheria inayosimamia na kukataa utesaji na vitendo vya utekaji,” amesema.
Mwanahakati wa haki za binadamu, Godlisten Malisa amedai matukio ya watu kupotea na kutekwa yameanza kurejea akimaanisha yalififia.
“Kwa siku za hivi karibuni matukio haya yameanza kurejea na kurudisha mashaka, wananchi wanataka kuona Serikali inakomeshaje matukio haya.
“Ukweli ni kwamba jamii inanyooshewa kidole kuhusu matukio haya,” amesema Malisa.
Kwa mujibu wa Malisa, ameitaka Serikali kuchukulia kwa uzito vitendo vya utekaji kwa kuunda Tume ya Kijaji kuchunguza matukio ya aina hiyo kwa kurejea miaka iliyopita na kutoa ushauri.
“Serikali iwachukulie wanaotoa taarifa za utekaji kama watu wema, sio kuwamakata, kwa sababu sio wahalifu bali itoe ushirikiano,”amesema Malisa.
Ofisa Uchechemuzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Maduhu William amedai watu wanaopotea ni wale wanaohoji baadhi ya vitu na baadaye hupatikana katika mazingira ambayo hakuna mtu anayejua walikuwa wapi.
Mchambuzi wa masuala ya Siasa, Luqman Maloto ameitaka Serikali kutoa majibu kuhusu matukio hayo yaliyoanza kujitokeza kuanzia mwaka 2016 hadi hivi karibuni ili kuonyesha namna inavyopambana na matukio hayo.
“Naamini jeshi la polisi linaweza kuonyesha kwamba linadhibiti vitendo hivyo, maana baadhi ya watekaji wanaojiona kama wapo peponi.
“Bunge lisimame imara kwa kukemea vitendo hivyo, haya matukio yameshawahi kujadiliwa bungeni,”amesema Maloto.
Akichangia mjadala huo, Mkazi wa Njombe, Anna Kanyika amesema ni vyema polisi akienda kukamata mtu atoe kitambulisho chake na si kukamata mtu na kuondoka naye.
Maelezo hayo ya Kanyika yalifanana na Bernard Semeni aliyedai hivi sasa Tanzania inaelekea katika uchaguzi, hivyo watu wanaodaiwa kuwa tishio kwa mtu fulani, basi wanakumbana na hali hiyo ili kumdhohofisha katika mchakato huo.
“Wananchi tunatakiwa kuwa mstari wa mbele kujitetea na kupaza sauti ili kuondokana na matukio haya, ikitokea mtu anakuja kukukamata lazima uumulize vitu vya muhimu vinavyotakiwa. Lakini Serikali itengeneze utaratibu maalumu utakaolinda raia wake,” amesema Semeni.
Suala la utekaji lilizungumziwa hivi karibuni na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba aliyesema:“Tuna matatizo ya watu kutekwa, na watu ambao wanaoitwa hawajulikana ni jamii hii, lakini kuna watu hawajulikani.”
“Huko nyuma kulikuwa na wakati mtu akiingia katika kijiji chochote kulikuwa na utaratibu wa kumfahamu,” alisema Jaji Warioba.
Aliongeza kuwa, “kulikuwa na utaratibu wa kufahamiana ili likitokea jambo tunasema inawekezana ni fulani, siku hizi huipati kwa sababu watu wana uoga kwa wananchi wa kawaida.”