Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive, imeamuru washtakiwa wawili kati ya 18 katika kesi ya ukahaba wakamatwe kwa kosa la kukiuka masharti ya dhamana.
Mahakama imefikia uamuzi huo baada ya washtakiwa hao na wadhamini wao kutohudhuria mahakamani.
Amri hiyo imetolewa leo Jumatano Julai 10, 2024 na Hakimu Mkazi Francis Mhina kutokana na ombi lililowasilishwa mbele yake na upande wa mashtaka.
Kesi hiyo ya jinai namba 17279 ya mwaka 2024, ilipangwa leo kwa ajili ya washtakiwa kusomewa hoja za awali baada ya upelelezi wa shauri hilo kukamilika.
Walioamriwa kukamatwa ni mshtakiwa wa 13, Diana David (23), na wa 17, Zainabu Hamis (21).
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo waliokuwapo mahakamani ni Amina Ramadhani, Mariana Sia, Mwajuma Hamza na Mariamu Hassan, Najma Hamisi, Mariam Kitamoga, Elizabeth Michael, Rosemary John, Jackline Daniel, Mwajuma Bakari, Jenifa John, na Recho Bakari.
Kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka moja la kufanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa ajili ya kufanya umalaya kinyume cha kifungu cha 176 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 na Marejeo ya mwaka 2022.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo Juni 14, 2024 maeneo ya Sinza Mori, wilayani Ubungo, Mkoa wa Dar es Salaam.
Washtakiwa wanadaiwa siku hiyo walikutwa wakifanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa kusimama hadharani, wakiwa wamevaa mavazi yasiyo ya heshima kwa lengo la kufanya umalaya.
Awali, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Regina Kayuni anayeshirikiana na Winifrida Wiko, aliomba Mahakama itoe amri ya kukamatwa washtakiwa hao kwa kukiuka dhamana.
“Tunaomba Mahakama yako itoa hati ya kukamatwa kwa washtakiwa hao ambao hawajafika mahakamani, lakini pia hawajatoa taarifa,” amedai Kayuni.
Wakili wa washtakiwa hao, Peter Madeleka anayeshirikiana na Gaston Garubindi amekubali ombi la upande wa mashtaka akieleza kama washtakiwa wamekiuka amri ya Mahakama hawana pingamizi.
“Hatuna pingamizi katika kutoa hati ya kuwakamata washtakiwa kwa sababu wamekiuka amri ya Mahakama, na ikae kwenye rekodi za Mahakama ikitokea upande wa wenzetu (upande wa mashtaka) wakashindwa kufika mahakamani, wasipate kigugumizi bali sheria ifuatwe kama ilivyofuatwa kwenye amri hii,” amedai Madeleka.
“Ikitokea mtu amedharau amri ya Mahakama, sheria ifuatwe kwa sababu na sisi tunakemea hilo na tunataka amri ya mahakama iheshimiwe,” amesema.
Hakimu Mhina baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, amekubali ombi la upande wa mashtaka na kutoa hati ya kukamatwa washtakiwa hao.
“Kwa washtakiwa ambao hawapo, Mahakama hii inatoa amri ya kuwakamata kama ambavyo upande wa mashtaka umeomba ili iwe fundisho kwa washtakiwa wengine kuheshimu amri ya mahakama,” amesema.
Mahakama baada ya kutoa amri hiyo, upande wa mashtaka uliwasomea hoja za awali washtakiwa.