India. Watu 18 wamepoteza maisha huku wengine 19 wakijeruhiwa nchini India baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuligonga lori la maziwa.
Ajali hiyo imetokea asubuhi ya leo Jumatano Julai 10, 2024 Kaskazini mwa Jimbo la Utter Pradesh nchini humo, polisi wamenukuliwa na Shirika la Habari la AFP.
”Basi hilo liligonga lori la mafuta kwa nyuma na kuua watu 18 na kuwaacha wengine 19 kujeruhiwa,” Zulfiqaar Ali, kutoka ofisi ya mkuu wa polisi wa wilaya, ameiambia AFP.
Inaelezwa basi hilo lilikuwa likielekea Mji Mkuu New Delhi kutoka Jimbo la Mashariki la Bihar, Shirika la Utangazaji la NDTV, limeripoti.
Hata hivyo, Al Jazeera imesema nguvu ya ajali imesababisha watu kutupwa nje ya gari na miili kutapakaa barabarani.
Mmoja ya kiongozi wa jimbo hilo, Brajesh Pathak amesema uchunguzi utafanywa ili kubaini sababu ya ajali hiyo.
Waziri Mkuu, Narendra Modi ametuma salamu zake za rambirambi akitumia mitandao ya kijamii na kutangaza fidia itakayotolewa na Serikali kwa waathiriwa na wapendwa wao.
Mei 2024, takriban watu 21 walifariki dunia na zaidi ya 50 kujeruhiwa wakati basi walilokuwa wakisafiria kudumbukia kwenye korongo kubwa huko Kashmir.
Imeandaliwa na Sute Kamwelwe