Wawili wafariki dunia kwa kunywa dawa ya kuacha pombe

Katavi. Watu wawili wa familia moja wamefariki dunia baada ya kunywa dawa ya kienyeji ili waache kunywa pombe kupindukia.

Tukio hilo lilitokea Julai 9, 2024 saa nne usiku katika Mtaa wa Kazima Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Jastin Patrick mjomba wa marehemu Paulo Mbalimba na Dismas Malimba amesema kutokana na unywaji pombe kupitiliza waliokuwa nao familia ilikaa na kujadili namna ya kufanya ili watu hao waache ndipo walipoamua kutafuta waganga watakaowapatia dawa.

“Ni kweli ndugu zetu wamefariki kwa kunywa dawa ya kuacha pombe maana walikuwa kama vichaa kitu ambacho kilifanya sisi wana familia kujadili namna ya kuwanusuru ndugu zetu na unywaji wa pombe za kienyeji kupitiliza,” amesema.

“Mganga wa kwanza alikuja akawafanyia dawa lakini haikusaidia kuacha tukaendelea kutafuta huku na kule tukapata mganga mwingine ambaye alikuja kuwatengenezea dawa wakanywa ghafla wakafariki dunia,”amesema.

Amesema mganga huyo wakati akiwapa dawa ndugu hao alikuwa haruhusu wanafamilia kushuhudia isipokuwa alikuwa akitoa taarifa ya kila kinachoendelea.

Patrick anasema kabla ya kuwapa dawa mganga aliuliza walikuwa wakitumia pombe gani akaambia gongo, wanzuki na komoni, aliagiza ziletwe ili azichanganye na dawa.

“Alichanganya pombe, asali mbichi na dawa kisha akazipasha moto baadaye akawapa wakanywa wakaanza kutapika na nguvu zikaanza kuwaishia akatuambia watapona lakini mwishoni akaja kutuambia ndugu zenu wamezimia kumbe tayari wamefariki wakati tunaenda kuwaangalia yule mganga alipata nafasi ya kutoroka na kutokomea kusipojulikana.”

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kazima Flavian Kisali amesema: “Ni kweli nimepokea taarifa ya watu wawili wa familia moja kwenye mtaa wangu wamepoteza maisha.

Amesema kwa mujibu wa familia, ilikuwa imechoka na tabia zao za kunywa pombe kupindukia ndipo wakaamua kutafuta waganga wa kienyeji awape dawa ili waache pombe.

“Niwaombe tu jamii hasa katika mtaa wangu mfahamu wapo watu kweli wanakunywa pombe hadi kero lakini ndugu wasiamini imani za kishirikina ambazo zinawafanya kusababisha kuleta madhara ya vifo na mambo mengine kwenye jamii,” amesema.

“Kikubwa inatakiwa tuwape elimu itakayowasaidia kuacha kunywa pombe lakini sio kuwapeleka kwa waganga wa kienyeji ambao wamekuwa matapeli wakubwa.”

Related Posts