Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko kwa miezi mitatu ya uongozi wake ndani ya wilaya hiyo, amekumbana na ukosoaji wa hatua mbili alizochukua ikiwamo oparesheni ya kutokomeza biashara ya ‘makahaba’ maarufu dada poa.
Operesheni hiyo ilipingwa kwa kile kilichoelezwa ukamataji uliofanyika unakiuka haki za binadamu na unaudhalilishaji.
Kadhia nyingine aliyokumbana nayo ni baada ya kuzungumza na wafanyabiashara walioitisha mgomo katika Soko la Mawasiliano Simu 2000, Ubungo na wafanyabiashara kumtaka aondoke kwa madai kuwa hawakuwa tayari kumsikiliza.
Mgomo huo ulilenga kupinga kile kilichoelezwa ni uamuzi wa Manispaa ya Ubungo kutangaza kulikabidhi eneo la soko hilo kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart).
Mambo hayo mawili ndiyo yamemkumba kiongozi huyo tangu alipohamishwa kutoka Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Machi 2024.
Mwananchi ilipomtafuta kuzungumzia matukio hayo aliyokumbana nayo kwenye uongozi wake, Bomboko amesema suala la ukamataji wa ‘makahaba’ maarufu dada poa ni kesi ambayo tayari ipo mahakamani.
“Sheria ndio itakuja kusema nani alikuwa sahihi tukisema sasa tutaharibu shauri lililopo mahakamani, tuiache Mahakama ifanye kazi yake,”amesema Bomboko.
Kuhusu machinga wa Soko la Simu 2000 amesema suala hilo lipo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila na yeye atalizungumzia vyema wiki ijayo.
Hatima ya suala hilo la wafanyabiashara litajulikana Jumamosi hii ya Julai 13, 2024.
Mtanzamo wa wakazi wa Ubungo
Mkazi wa Kimara, Enock Japhet akizungumzia ukosoaji anaoupitia Bomboko, amesema: “Hakuna alichokosea, ukiangalia kabla ya kutangaza operesheni hiyo na kuwakamata wahusika, hao kina dada walijiachia sana waliona hakuna sheria yoyote ya kuwashughulikia sasa kitendo cha kuchukuliwa hatua ndio unasikia watu wanapiga kelele lakini hata hao wanaopiga kelele hizo biashara hawazipendi.”
Kuhusu machinga kumsikiliza kiongozi huyo amesema mambo mengine yapo kisiasa.
“Hakuna sababu ya kukataa kumsikiliza kiongozi kama kuna jambo ambalo lipo tofauti na limefanywa na Serikali yeye ndiye atarudi kusema kilichofanyika sio sawa na hii ni baada ya kuwasiliza malalamiko yenu,” amesema.
Kwa upande wake, Jasmin Rashid mkazi wa Mbezi Louis amesema biashara ya ngono haikubaliki na hatua zilizochukuliwa na kiongozi wao ndio kilio cha muda mrefu ya wananchi.
“Suala la ukahaba tumelipigia kelele kwa muda mrefu kwahiyo tulipoona hatua zikichukuliwa tulifurahi, mtu anayepinga operesheni hii ana lengo lake binafsi kwa sababu kama mtu anakiuka maadili lazima mamlaka zilizopo zimuwajibishe,”amesema.
Naye Aisha Abdul amesema suala la machinga kutokubali kumsikiliza mkuu wa wilaya wakati wa mgomo ni kutokana na viongozi wa wilaya hiyo kuhusika kupanga njama ya kuwaondoa kwenye maeneo yao kwa lengo la kuyagawa.
“Wafanyabiashara waliona tangazo la kutoka Wilaya ya Ubungo kwamba wataondolewa Soko la Simu 2000, wasingekubali kuongea na watu hao waliopanga kuwaondoa bila kuwashirikisha ndio maana walimkatalia kiongozi huyo, mkuu wa wilaya anapaswa tu kufahamu katika maamuzi yote yatakayofanyika yawe shirikishi,”amesema Abdul.
Juni mwaka huu, Bomboko aliendesha operesheni ya kusaka na kuwakamata kina dada wanaofanya biashara ya ngono pamoja na wateja wao na kuwasweka rumande.
Katika operesheni hiyo, ‘makahaba’ walikamatwa maeneo ya Ubungo, River Side na Sinza, hali iliyovuta wanaharakati wa haki za binadamu wakieleza kuwa kitendo kilichotendeka kinaingilia faragha za watu na kinakiuka haki za binadamu.
Baada ya tukio hilo, watuhumiwa 36 walilalamika kudhalilishwa hivyo wakili wao Peter Madeleka alipeleka notisi ya wateja wake kwa mkuu huyo wa wilaya kulipwa Sh36 bilioni kwa kudhalilishwa kuitwa ‘dada poa’ na kuwaweka rumande kwa zaidi ya siku tano kinyume na sheria.
Kesi ya wanawake hao kufanya biashara ya ngono tayari imepelekwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive.
Sakata la pili lililoibua ukosoaji kwa kiongozi huyo ni uamuzi wa Manispaa ya Ubungo kutoa tangazo Julai 4, 2024 la kulikabidhi eneo la Soko la Mawasiliano Simu 2000 kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) baada ya kikao cha Baraza la Madiwani.
Baada ya wafanyabiashara hao kuandamana na mkuu huyo wa wilaya kufika eneo la tukio waandamanaji walimtaka aondoke.
Hata hivyo, kiongozi huyo akizungumza na waandishi wa habari amesema hoja inayotolewa kuwa soko hilo limeuzwa kwa Wachina hazina ukweli.
“Kuna siasa ambazo mavuguvugu haya yameanza maeneo mengi, miaka saba nyuma soko hili walijengewa vibanda vya kudumu, mmiliki wa eneo hili ni Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, kama Meya na Mwenyekiti wa Halmashauri hawajawahi kufanya kikao na wafanyabiashara hizi nyingine ni vurugu,” amesema.